Mkwara wake lazima Msuva na Ngassa watulie

Muktasari:
Hata hivyo, Geofrey Mwashiuya, winga mpya wa Yanga anajipa moyo kuwa, mradi ametua Jangwani, yupo tayari kukabiliana na ushindani wowote wa namba.
ANAUJUA ukali wa Simon Msuva. Kinara wa mabao katika Ligi Kuu ya msimu huu. Anaujua muziki wa Mrisho Ngassa, nyota wa kimataifa ambaye kwa karibu muongo mmoja anatetemesha Tanzania.
Hata hivyo, Geofrey Mwashiuya, winga mpya wa Yanga anajipa moyo kuwa, mradi ametua Jangwani, yupo tayari kukabiliana na ushindani wowote wa namba.
Chipukizi huyo aliyesajiliwa mwishoni mwa mwaka jana, anasema anajua mwanzo utakuwa mgumu kwake, lakini kwa vile anajiamini na soka analiweza, atakula sahani moja na wakali hao wa Jangwani.
“Ni kawaida katika maisha, mwanzo huwa mgumu, ila kwa imani yangu nitatimiza malengo yangu kwa sababu najitambua. Ushindani wa namba ni mkubwa, lakini nitajituma katika mazoezi na kushirikiana vizuri na wenzangu ili kazi yangu iwe nyepesi mno kikosini,” anasema Mwashiuya.
Mchezaji huyo aliyesajiliwa kutoka Kemondo ya mjini Mbeya, anasema anajiona ni mwenye bahati kuweza kusajiliwa na Yanga kisha kutua moja kwa moja katika timu ya wakubwa.
Ingawa bado hajaanza kucheza katika ligi hadi msimu ujao, lakini ameonyesha ni mchezaji anayejiamini na mwenye mambo mengi ambayo Yanga haitajutia fedha ilizotoa kumsajili.
“Najiona mwenye bahati kwani nimeingia Yanga yenye wachezaji wazuri ambao kwangu watakuwa ni taa ya kuongoza kipaji changu. Nitajifunza mengi kutoka kwao sababu wao ni wazoefu.
“Lakini napenda wapenzi na wanachama wa Yanga watambue, nimekuja kikosini kucheza. Nitacheza kwa uwezo wangu wote ili kuwafurahisha. Kikubwa ninachokiomba ni ushirikiano tu kutoka kwa wachezaji wenzangu, viongozi na mashabiki, pia wanipe muda kuzoea mazingira.”
Ndoto
Mwashiuya anasema Yanga imetimiza sehemu ya ndoto zake alizokuwa akiziota tangu utotoni ya kuja kuchezea klabu kubwa ya soka nchini.
Winga huyo mwenye umri wa miaka 19, anasema Yanga ni moja ya klabu kubwa ambayo kila mchezaji hutamani kuichezea na anashukuru kuweza kutimiza jambo hilo baada ya kusajiliwa.
Anawaambia mabosi wake wa Yanga wajiandae kula matunda ya kusajiliwa kwake kwa sababu akili yake ni kuhakikisha anakipa heshima kikosi hicho kama sehemu ya kulipa fadhila.
Maisha ya soka
Mwashiuya aliyezaliwa na kukulia Mbozi, Mbeya anasema kipaji chake cha soka ni cha kuzaliwa nacho kwani amekirithi toka kwa baba yake mzazi Bahati Mwashiuya aliyekuwa kipa enzi za uchezaji wake hata kama hakufika mbali kimafanikio.
Anasema tangu akiwa mdogo alipenda kucheza, lakini alianza kufahamika baada ya kujiunga na Shule ya Msingi Lutumbi.
“Nilipojiunga na Sekondari ya Nalielie na kukutana na vijana mbalimbali, kipaji changu kiliendelea kukua na kuchaguliwa timu ya shule na kushiriki mashindano kama ya Umiseta. Baada ya kufanya vizuri nilichaguliwa kuunda kombaini ya wachezaji wa Shule za Nyanda za Juu Kusini kwa ajili ya kushiriki mashindano ya taifa ambayo yalifanyika Kibaha.
“Nakumbuka ilikuwa mwaka 2011 nikiwa kidato cha pili. Mashindano yale yalikuwa ni bahati kwangu kwa sababu nilionekana na kujulikana zaidi kiasi cha kufuatwa na mwalimu wa Makongo, Oscar Milambo aliyevutiwa nami na kunishawishi kujiunga na shule yake,” anasema.
Mwashiuya anasema akiwa Makongo alipata fursa ya kusoma na kucheza soka pamoja na Edward Charles na Amos Abel ambao wote ni mabeki wa kushoto wa Yanga.
Anasema, baada ya kumaliza masomo yake, alirudi kwao Mbeya na kusajiliwa na Kimondo na kushiriki nao katika michuano ya Ligi Daraja la Kwanza. Wakiwa katikati ya msimu ndipo Yanga walipomwona na kumsajili rasmi.
Anadokeza kuwa kusajiliwa kwake Yanga hakuna maana kwamba ameridhika na mafanikio. ”Hapa siyo mwisho wa safari yangu. Malengo yangu ni kucheza mpira wa mafanikio kwenye klabu zilizoendelea, lakini yote ninamwomba Mungu anipe uzima nisikumbane na majeraha.”
Mwashiuya anasema kabla ya kutua Yanga, aliwahi kuchezea timu yake ya mtaa ya Hollywood iliyokuwa inashiriki mashindano mbalimbali ya wilaya na mkoa.
Simba, Azam zammendea
Mwashiuya anasema kabla ya kunyakuliwa na Yanga, klabu za Simba na Azam zilikuwa zikimnyatia kumnasa.
“Kabla sijaja Yanga, timu nyingi zilikuwa zikinihitaji ikiwemo Simba na Azam, ila Yanga walikuwa na bahati ya kuninasa. Ni moja ya timu kubwa na sikusita waliponitwangia simu kunieleza wananitaka,” anasema.
Asilosahau
Mwashiuya anasema, katika maisha yake ya soka, japo hana muda mrefu, lakini hawezi kusahau tukio lililowahi kumtokea uwanjani akiwa na timu yake ya mtaani ya Hollywood.
Anasema tukio hilo ni lile la kupigwa na mchezaji mwenzake na kusababisha azimie kiasi cha kudhaniwa amekufa.
“Wakati naichezea Hollywood katika michuano ya Ligi ya Wilaya, tulicheza na Boma Uwanja wa Magereza pale Mbeya. Nikiwa katikati ya mchezo, nilipigwa na mchezaji mwenzangu bila hata kosa. Nilizimia kwa muda wa saa moja jambo lililowashtua ndugu na jamaa zangu ambao walidhani nimekufa.”
Nje ya soka
“Kwangu, mazoezi ndiyo kila kitu. Natumia muda wangu mwingi kufanya mazoezi. Na ninapotulia nyumbani huwa napenda kubadilishana mawazo na jamaa zangu. Siyo mpenzi sana wa muziki ingawa mara chache huwa anasikiliza na msanii ninayemzimia ni Ally Kiba,” anasema.
Juu ya misosi, Mwashiuya anasema anauzimia sana mlo wa wali kwa samaki, pia hutumia vinywaji laini.
Pluijm anena
Baada ya kushuka Mwashiuya mazoezini, Kocha Hans Pluijm hakusita kusema; ”Mwashiuya ni mchezaji mzuri, kama atajitambua na kujitunza kwa hakika atakuja kuisaidia Yanga hapo baadaye. Ni kijana mdogo ambaye anahitaji muda kwa sasa ili apate uzoefu zaidi.”
Akizungumzia nafasi yake kikosini, Pluijm anasema: “Mwashiuya ni winga halisi wa kushoto, hiyo ndiyo nafasi ambayo ukimpa majukumu atakufanyia kazi yako kwa ufasaha.”
Baadhi ya mashabiki na hata wachezaji wenzake wamemfagilia na kumtabiria kufika mbali, cha muhimu kwake ni kuhakikisha havimbi kichwa ili kutimiza tabiri hizo na kuja kufanikiwa kisoka.