Mkali wa Black Panther kuja kufundisha kuogelea

Muktasari:
- Wade ambaye pia mwigizaji wa filamu za Hollywood ikiwamo ya Black Panther-Wakanda Forever iliyotoka mwaka 2022 ataendesha mafunzo hayo ya kuogelea nchini akishirikiana na Champion Rise Sports Promoter.
KOCHA maarufu wa mchezo wa kuogelea duniani, Atiba Hasim-Nii Wade kutoka Marekani anatarajiwa kutua nchini ili kuendesha mafunzo ya mchezo huo kuanzia Juni 27 hadi Julai Mosi.
Wade ambaye pia mwigizaji wa filamu za Hollywood ikiwamo ya Black Panther-Wakanda Forever iliyotoka mwaka 2022 ataendesha mafunzo hayo ya kuogelea nchini akishirikiana na Champion Rise Sports Promoter.
Mbali na filamu ya Black Panther, Wade ameigiza pia Kaleidoscope (2023) na Pride (2007) na Mkurugenzi wa Champion Rise, Amina Mfaume alisema nyota huyo ataendesha pia kozi ya kimataifa ya makocha wa mchezo huo inayotambulika na Chama cha Makocha wa Kuogelea Marekani (ASCA).
Mafunzo hayo yafanyika kati ya Julai 1-7 na Amin alisema kuwa lengo la kozi hiyo ni kuinua viwango vya makocha wa kuogelea hapa Tanzania.
“Mpango huu utaanza kwa mafunzo ya waogeleaji ambapo wanamichezo chipukizi watafaidika moja kwa moja na ujuzi wa kocha Wade katika kuboresha mbinu za kuongeza. Baada ya mafunzo ya waogeleaji, itafuata kozi ua makocha ambayo ni fursa ya kipekee kwa makocha,” alisema Amina.
Amina alifafanua, kocha Wade ni mtu mashuhuri katika mazoezi ya utendaji wa hali ya juu na mbinu mbalimbali, kwani mbali na umahiri wake kama kocha aliyeidhinishwa na ASCA, Wade pia ana uzoefu wa kipekee unaojumuisha michezo na filamu.