Mitutu nje nje.. Ulimwengu azua jambo DR Congo

Tuesday May 04 2021
mitutu pic
By Eliya Solomon

NYIE acheni kabisa. Unaambia huko DR Congo hali ya hewa ilichafuka hadi mitutu ikabidi itumike baada ya mshambuliaji wa TP Mazembe na Taifa Stars, Thomas Ulimwengu kutupia bao kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Sanga Balende.

TP Mazembe ambao wanapambana kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu DR Congo yamewakuta majanga hayo wakiwa ugenini dakika za mwisho kabisa kabla ya mchezo huo ambao waliibuka na ushindi wa bao 1-0 kumalizika.

Kilichotokea ni kwamba mashabiki wa Sanga Balende waliona mwamuzi wa mchezo huo amewaonea baada ya kuwanyima penalti hivyo kitendo cha TP Mazembe kupata bao dakika za mwisho lililofungwa na Ulimwengu ndio kikachochea zaidi hasira zao.

Walichukua maamuzi mkononi kwa kuanza kurusha mawe uwanjani, vurugu zilitokea kwa zaidi ya dakika tatu, ikabidi watu wa usalama waingilie kati na kupiga risasi juu ili kuwatawanya mashabiki hao ambao walionekana kuwa na hasira kali.

Ilibidi wachezaji wote wa TP Mazembe wabebwe na gari maalum la kijeshi na kuondolewa uwanjani hapo kisha kusindikizwa hadi nje ya mkoa huo na kurejea nyumbani wakiwa na maumivu, inaelezwa ni wachezaji watatu ambao walipata majeraha.

Upande wake Ulimwengu alitueleza, “Nipo poa sikupata majeraha yoyote.”

Advertisement
Advertisement