Metacha aanza, Polisi Tanzania ikitakata mbele ya Alliance FC

Muktasari:

  • Polisi Tanzania wataianzaLigi Kuu msimu wa mwaka 2021-2022 kwa kuikaribisha KMC ya Dar es Salaam Septemba 29, mwaka huu saa 8 mchana katika uwanja wa Ushirika mjini Moshi.

Mlinda Mlango mpya wa Polisi Tanzania, Metacha Mnata leo ameanza rasmi kuitumikia timu yake baada ya kucheza mchezo wa kwanza akiwa na maafande hao katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Alliance FC ya Mwanza.

Mchezo huo wa pili wa kirafiki kwa maafande hao umechezwa leo katika uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa huku Polisi Tanzania wakiibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa mnamo dakika ya 39 na Adam Adam.

Katika mchezo huo Metacha alidaka kwa dakika 45 akiisaidia timu yake kumaliza kipindi cha kwanza wakiwa wanaongoza kwa bao 1-0 lakini kipindi cha pili alipumzishwa na nafasi yake kuchukuliwa na Msafiri Mkumbo.

Metacha ambaye alichelewa kujiunga kwenye kambi ya timu hiyo kutokana na majukumu ya timu ya taifa aliripoti usiku wa Septemba 10 na kufanya mazoezi ya pamoja na timu Septemba 11 (Jumamosi) timu hiyo ilipocheza mechi yake ya kwanza ya kirafiki jijini hapa dhidi ya Mwanza Kombaini na kukubali kichapo cha mabao 2-1.

Vile vile, beki mpya Said Juma 'Makapu' alicheza dakika 45 na kumpisha mkongwe na mchezaji mwenzake wa zamani wa Yanga, Kelvin Yondani aliyeendelea kuimarisha ulinzi wa maafande hao na kumaliza dakika 90 bila wavu wao kuguswa.

Metacha ameiambia Mwanaspoti Online kuwa amefurahishwa na mapokezi aliyoyapata ndani ya kikosi hicho huku akiwa na matumaini kuwa timu yao itafanya vizuri kwani maandalizi yanayofanywa kwa sasa yanaonyesha namna timu hiyo ilivyodhamiria kushindana.

Timu hiyo imeendelea kujifua katika kambi yake ya siku 14 jijini hapa ikijiandaa na Ligi Kuu itakayoanza Septemba 27, mwaka huu, ambapo Polisi wataanzia nyumbani Ushirika Moshi Septemba 29 watakapoialika KMC ya Kinondoni.

Katika kambi hiyo Polisi tayari wamecheza mechi mbili dhidi ya Mwanza Kombaini na Alliance huku wakiwa na ratiba ya kukipiga na Geita Gold Septemba 16 (Alhamisi) katika uwanja wa CCM Kirumba kabla ya kurudi mkoani Kilimanjaro.