Messi vs Ronaldo : Ronaldo amkataa Rafa Benitez Real Madrid
Muktasari:
Hakika sifa zake zinazungumza zenyewe, lakini haikuchukua muda ikabainika wazi kwamba kuna mahala jambo halikuwa likienda vizuri. Benitez na wachezaji wake hawakuwa na maelewano mazuri.
TOLEO ililopita, mwandishi, Luca Caioli alielezea jinsi Ronaldo alivyolia baada ya Ureno kulikosa taji la Euro 2004 nyumbani pamoja na ujio wa kocha mpya katika klabu ya Real Madrid, Rafa Benitez. Endelea…
Kama ilivyokuwa ikisemwa, Benitez ni wale watu wanaoitwa Madridista wa ukweli kutoka moyoni, alianzia maisha yake ya kucheza soka la ushindani na ukocha katika ligi ya vijana akiwa na Real Madrid.
Na sasa anarudi kivingine akiwa na rekodi ya kutwaa mataji mawili ya La Liga na Valencia na Ligi ya Mabingwa, Kombe la FA, Ngao ya Jamii akiwa na Liverpool, taji la Uefa akiwa na Chelsea pamoja na Italia Supercup na Kombe la Dunia la klabu akiwa na Inter Milan na Coppa Italia akiwa na Napoli.
Hakika sifa zake zinazungumza zenyewe, lakini haikuchukua muda ikabainika wazi kwamba kuna mahala jambo halikuwa likienda vizuri. Benitez na wachezaji wake hawakuwa na maelewano mazuri.
Hapo hapo kukawa na uvumi kwamba alikuwa akiwabana mno, alikuwa akitaka kuweka mazingira ya nidhamu ambayo yangemfanya awe na mamlaka kamili katika kila kitu.
Hata hivyo, mpango wake huo haungewezekana hasa kwa kuwa alikuwa akiongoza orodha ndefu ya mastaa wenye mishahara mikubwa wenye tabia ya kufanya mambo mengi au machache kadri walivyoona inafaa.
Moto ukaanza kuwaka kwa kasi na zaidi kukawa na tatizo kati yake na Ronaldo ambaye tofauti zao zilijitokeza zaidi ya mara moja kwenye mazoezi.
Tangu kuwasili, Benitez akawa anaulizwa mara kwa mara anafikiria nini kuhusu Ronaldo, lakini hakuwa na jibu la moja kwa moja alikuwa mwenye kuzunguka.
Mara ya kwanza aliulizwa akiwa katika ziara ya maandalizi ya ligi nchini Australia ambako alisema,
“Nilikuwa na bahati mbaya ya kukutana naye na kutofautiana akiwa England wakati huo mimi nikiwa na Liverpool, alikuwa na mchango mkubwa kwenye timu.
“Kwa sasa amekuwa zaidi na mzoefu na nafikiri inatosha tu kusema yeye ni mmoja wa wachezaji bora duniani,’’ alisema Benitez.
Alipoulizwa tena wiki chache zilizofuata alifunguka zaidi lakini hakwenda mbali, “Nafikiri ni mchezaji mzuri, mmoja wa wachezaji bora niliowahi kuwafundisha, siwezi kusema yeye ni bora kwa sababu nina bahati ya kufanya kazi na wachezaji wengi wazuri lakini nikizungumzia wakati huu, yeye anabaki kuwa mchezaji wetu bora na ndiye bora duniani.”
“Kwa nini hukiri tu kwamba Ronaldo ni bora? Mmoja wa waandishi aliuliza swali hilo Septemba 16 baada ya mechi na Shakhtar Donetsk.
“Nashangaa uko makini mno na nini mtu mmoja anafikiria kuliko yanayoendelea uwanjani,’’ alijibu Benitez akionyesha wazi namna ambavyo hakuwa tayari kuficha shauku yake ya kumaliza maswali ya aina hiyo.
“Ronaldo ni bora duniani najua uwezo wake anauonyesha katika kila mechi na kila anapofanya mazoezi, ni bora dunian, kuanzia sasa nitasema ndio kwa kila mtakachoniuliza halafu baada ya hapo tutaendelea kujadili anachofanya uwanjani,” alisema Benitez.
Hata hivyo, kilichoonekana ni kama vile alikuwa akizungumza tu kumaliza mazungumzo, vyombo vya habari na hata mashabiki waliamini Real Madrid ilikuwa hovyo na wako waliojenga hisia kuwa huenda hata wachezaji walikuwa hawaitumikii timu kikamilifu kama aina ya mgomo baridi kwa kocha wao mpya.
Kwa mara ya kwanza tangu awasili katika timu hiyo, kukawa na maneno ya mara kwa mara kutaka auzwe katika klabu nyingine kwa bei nzuri.
Mambo yakazidi kuwa moto baada ya mapumziko ya Krismasi, Benitez akatimuliwa na Zinedine Zidane akawa kocha mpya, Ronaldo hakuona sababu ya kuficha kuridhishwa kwake baada ya tukio la kutimuliwa Benitez kutangazwa hadharani.
“Tumepoteza muda mwingi katika jambo hili,’’ aliliambia gazeti moja na baada ya msimu wa La Liga na baada ya Benitez kutimkia Newcastle. Moja ya sababu za kutofautiana kati ya Benitez na Ronaldo ni kitendo cha Benitez kusisitiza kumfundisha Ronaldo namna ya kupiga mipra ya adhabu.
“Kuna aina ya mambo ambayo huwezi hata kujadiliana na mtu ambaye ana mawazo tofauti na yako, unaishia tu kuwashukuru na kuendelea na yako, kuna mambo ya kujifunza kutoka kwa kila kocha lakini yapo ambayo ni ama unayo au hauna,’’ alisema Ronaldo.
“Ananifundisha mimi kuhusu mipira ya adhabu lakini pia namna nzuri ya kushambulia na mpira na namna ya kupiga chenga.”
Ushauri wa aina hiyo Ronaldo hakukubaliana nao, ni matukio ambayo aliamua kuyageuza hatua ambayo mchezaji huyo angependa kuyasahau.
Itaendelea Jumanne ijayo…