Messi vs Ronaldo : Messi apigwa madongo kila kona
Muktasari:
Mwaka mmoja baadaye habari inayofanana na hiyo ikajitokeza pale alipopewa tuzo ya mwanasoka bora wa Copa America, lakini safari hii hakwenda kuchukua tuzo yake.
KATIKA toleo lililopita, Mwandishi, Luca Caioli alizungumzia hali ilivyokuwa baada ya Messi kushindwa kuisaidia Argentina kubeba Kombe la Dunia kule Brazil mwaka 2014 na hali ya unyonge ilivyomtawala mchezaji huyo. Endelea…
Baada ya kuanza vizuri fainali za Brazil, Messi aliishia kurudi nyumbani mikono mitupu, kweli alitwaa tuzo ya kiatu cha dhahabu akiwa mchezaji aliyeng’ara katika mashindano hayo, lakini pamoja na uzuri wake ilikuwa kama haina maana.
Zaidi ya hilo kukawa na mijadala yenye utata kuhusu Messi iwapo alitakiwa hata kupewa tuzo hiyo, baadhi ya watu akiwamo Maradona mwenyewe alisema kwamba timu ya watu 13 walioteuliwa na Fifa kufanya uamuzi huo waliangalia umaarufu na si ubora.
Akiwa hajui shutuma zilizokuwa zikitolewa au akiwa amehisi kuna utata unaomzunguka, Messi hakutaka kujaribu hata kutabasamu kidogo wakati akienda kuchukua tuzo yake. Ilikuwa ni dakika kadhaa chache baada ya Nicola Rizzoli kupuliza filimbi ya kumaliza mchezo wa fainali. Kichwa chini Messi alikuwa akijaribu kukifanyia tathmini kile kilichotokea katika Uwanja wa Macarana mjini Rio de Janeiro.
Hata hakujihangaisha kumuangalia usoni kipa na mshindi wa ‘glovu za dhahabu’ Manuel Neuer wakati wakisalimiana kwa kupeana mikono kabla ya kwenda kupiga picha ambalo ni tukio la lazima.
Lilikuwa ni tukio la aina yake, uso wake aliuweka chini akiangalia nyasi za uwanja, Messi alionekana mdogo mno kuzidiwa na kipa huyo wa Ujerumani na pia alionekana hayuko katika utulivu bila kusahau ukweli kwamba matukio ya mechi hiyo ni kama vile yaliendelea kujirudia kichwani mwake.
Hakuona tabu kuficha huzuni aliokuwa nayo mbele ya vyombo vya habari, “Sijali kuhusu hii tuzo ya mpira wa dhahabu bali nilichokitaka ni kubeba Kombe la Dunia.”
Mwaka mmoja baadaye habari inayofanana na hiyo ikajitokeza pale alipopewa tuzo ya mwanasoka bora wa Copa America, lakini safari hii hakwenda kuchukua tuzo yake.
Ilikuwa ni Julai 4, 2015, na kwa mara nyingine, Argentina ilikuwa karibu kutwaa taji, lakini ikashindwa fainali kwa mara ya pili mfululizo na hivyo hakutaka kuingia tena katika mtego wa kuibua utata kwa mara nyingine kwa kukubali tuzo binafsi.
Zaidi ya hilo pia alionekana kutokuwa katika hali ya utulivu wakati akienda kupokea medali kwa kushika nafasi ya pili akiwa na wachezaji wenzake, akaivua mara tu baada ya kuvalishwa shingoni.
Safari hii Argentina ilifungwa na Chile ambayo ilikuwa mwenyeji wa mashindano.
Kama ilivyokuwa Rio de Janeiro, Messi hakuwa na mchango mkubwa kwa timu yake uwanjani katika mechi hiyo hadi mechi inamalizika na timu kwenda kwenye mikwaju ya penalti.
Alikuwa akikabwa mwanzo mwisho wakati wote wa mechi na baadhi ya mashabiki wa Chile jukwaani wakawa wakiishutumu na kuidhihaki familia yake na ilipokuja kwenye mikwaju ya penalti, Messi alifanikiwa kuujaza mpira wavuni wakati wachezaji wenzake, Higuan na Banega wakakosa.
Pamoja na yote hayo mashabiki wa Argentina wakamuangushia lawama zote Messi, ilikuwa sawa na hadithi ya kushushiwa jumba bovu, alijikuta akisakamwa kwenye vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii.
Gazeti maarufu la 0le lilikwenda mbali zaidi kwa kumtaka Messi ajivue unahodha wa timu hiyo na kama ilivyo ada Maradona naye akawa na cha kusema, “Tuna mwanasoka bora duniani, ambaye anakwenda kufunga magoli manne dhidi ya Real Madrid. Na huyo huyo anakuwa wa kuzungukazunguka na kuugusa mpira mara chache. Niambie wewe ni Muargentina au Msweden?”
Hata hivyo, baadaye Maradona ni kama alichoshwa na mambo ya Messi akahitaji apewe utulivu pale aliposema: “Messi anatakiwa kuchukuliwa kama mchezaji mwingine ambaye anavaa jezi ya timu ya taifa, ndio yeye ni mchezaji bora duniani, kwa mazuri au mabaya lakini sikilizeni hajaua mtu, hajabaka mtu tusigeuze hii kama michezo ya kuigiza majukwaani.
Itaendelea Jumamosi ijayo