Messi vs Ronaldo : mambo magumu yamwandama Messi, familia yake Barcelona

Muktasari:
Kuna ambao walimuona Messi kuwa ni mdogo mno na asiye na nguvu na kushangaa kwa nini kunakuwa na mjadala kuhusu mchezaji ambaye yuko katika hali hiyo na zaidi ya yote umri ulikuwa mdogo sana na walitakiwa kutafuta aina ya ajira yenye manufaa kwa wazazi wake.
TOLEO lililopita, Mwandishi, Luca Caioli alichambua jinsi ubora wa Messi ulivyoonekana hadi harakati za kumsajil Barcelona kuanza kutokana na kiwango chake cha soka la kuvutia. Sasa endelea…
“Nini hiki nimeona, mtoto ambaye alikuwa na umbo dogo lakini yuko tofauti ana hali ya kujiamini ya ajabu mwepesi, makini ana kasi na mwenye uwezo wa kumhadaa yeyote atakayejitokeza mbele yake, haikuwa vigumu kuyaona hayo, kuona kipaji chake ambacho kwa sasa kimejulikana kwa kila mtu, kimeonekana zaidi akiwa na miaka 13.
“Kuna wachezaji wanaohitaji timu ili wang’are lakini si yeye, kwa wote ambao wananiambia mimi kwamba ndiye niliyemvumbua Messi wakati wote huwa nawajibu, “Hata watu wanaoishi katika sayari nyingine wakimuona watakubali kwamba ni mtu wa kipekee.
Bosi tayari alishaona kila kitu na kukubali na hivyo kulichobaki ilikuwa ni kukamilisha dili, lakini hapo hapo likaja suala lenye utata, kwanza walitakiwa kumaliza mambo ya msingi katika kusaini mkataba na si kila mtu katika klabu alishawishika.
Kuna ambao walimuona Messi kuwa ni mdogo mno na asiye na nguvu na kushangaa kwa nini kunakuwa na mjadala kuhusu mchezaji ambaye yuko katika hali hiyo na zaidi ya yote umri ulikuwa mdogo sana na walitakiwa kutafuta aina ya ajira yenye manufaa kwa wazazi wake.
Na matatizo hayakuonekana baada tu ya mkataba kusainiwa, miezi ya kwanza ya maisha yake mapya kwenye ardhi ya Barcelona hayakwenda vizuri.
Machi 6, 2001, Messi alipata leseni ya awali ya mchezaji lakini alikuwa mtu wa taifa jingine, hangeweza kucheza mashindano ya kitaifa na hivyo asingeweza kuungana na timu A ya watoto ya Barcelona ambayo ndiyo iliyokuwa timu yake.
Kutokana na hali hiyo alipelekwa timu B na maana yake ni kwamba aliishia kucheza mashindano ya mikoani au majimbo, kama hiyo haitoshi hali ikawa mbaya zaidi kwani tayari timu zilishaandaliwa na zilikuwa mashindanoni.
Na pamoja na umahiri wa Messi bado isingekuwa jambo zuri kumuondoa au ‘kumtoa kafara’ mtoto yeyote kwa ajili yake hasa watoto ambao tayari walishaanza kucheza tangu mwanzo mwa msimu wa ligi eti kwa sababu tu ya kumpa nafasi Messi.
Jambo jingine ni kwamba klabu yake ya zamani ya Newell ya Argentina haikuwa na utayari katika kuzifanyia kazi taratibu za utoaji wa cheti cha uhamisho ili Barcelona iwe na uhalali wa kummiliki kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka Hispania.
Kama hiyo haitoshi bado kukawa na majanga mengine, Aprili 21, Messi akiwa uwanjani alichezewa rafu mbaya na kuumia mguu wa kushoto, ni majeraha ya mara ya kwanza makubwa kwa Messi katika maisha yake ya soka.
Ni majeraha ambayo yalimuweka nje ya uwanja hadi Juni, kwanza alihitaji kuwekewa kifaa maalumu cha kuushikiza mguu na baada ya hapo akafungwa POP.
Wiki moja baadaye likatokea jingine, majeraha mengine, safari hii aliyapata wakati akishuka kwenye ngazi, aliumia enka ya mguu wa kushoto, bahati maumivu haya hayakuwa makubwa sana, alikaa nje ya uwanja kwa wiki tatu.
Maisha yake ya Barcelona ni kama yalianza na majanga, ni kama vile aliingia na mguu usio sahihi hali haikuwa nzuri kiasi kwamba katika msimu huo mmoja, kutokana na mlolongo wa matatizo, Messi alicheza mechi mbili tu za mashindano, na moja ya kirafiki.
Mbali na majanga hayo, Messi na familia yake walijikuta walikabiliana na changamoto nyingine japo mambo hayakuwa magumu sana kwa Messi ila mdogo wake wa kike, Maria Sol alikuwa na wakati mgumu kuendana na maisha mapya.
Hali hiyo iliifanya familia kuchukua uamuzi mgumu wa kuondoka miezi mitano baada ya kuwasili, mama wa Messi, Celia alilazimika kurudi Argentina na Maria Sol wakati Jorge alibaki Barcelona na watoto wa kiume.
Itaendelea Jumanne ijayo…