Mdamu aanza kupata msaada "angalau nitapata chakula"
Muktasari:
- Julai 9, mwaka 2021 basi la timu ya Polisi Tanzania, lilipata ajali likitoka katika mazoezi Uwanja wa TPC kuelekea kambini, ambapo Mdamu alivunjika miguu yote miwili, jambo ambalo liliwagusa Watanzania kadhaa kujitoa kwa ajili ya matibabu yake.
BAADA ya Mwanaspoti kufichua hali ya maendeleo ya aliyekuwa mshambuliaji wa Polisi Tanzania, Gerald Mathias Mdamu kuhitaji msaada wa matibabu na mahitaji binafsi, wadau kadhaa wameanza kujitolea kumtatulia baadhi ya changamoto na ameshukuru kwamba ; "angalau sasa nitapata chakula"
Julai 9, mwaka 2021 basi la timu ya Polisi Tanzania, lilipata ajali likitoka katika mazoezi Uwanja wa TPC kuelekea kambini, ambapo Mdamu alivunjika miguu yote miwili, jambo ambalo liliwagusa Watanzania kadhaa kujitoa kwa ajili ya matibabu yake.
Kwa mdau au taasisi inayopenda kumsaidia Mdamu kwa fedha, vifaa tiba au matibabu wawasiliane naye mwenyewe kupitia namba yake;
0655-670101
(itasoma Juliana Malekel)
Mwanaspoti lilimtembelea Mdamu nyumbani kwake Kimara Bonyokwa, jijini Dar es Salaam juzi, lilijionea hali halisi, huku paja la mguu wa kushoto lilikuwa likivuja usaha.
Wadau mbalimbali wa soka nchi, walipoona taarifa hiyo kupitia Mwanaspoti leo wameanza kuguswa na hali yake, hivyo baadhi yao wameanza kumtumia kiasi kidogo cha fedha ambacho amekiri kuwa kitampa mlo wa leo na kesho huku akizidi kuomba Mungu apate kiasi cha kufanikisha matibabu yake haraka iwezekanavyo.
Mdamu amezungumza na Mwanaspoti mchana huu na kusema "Ni zaidi ya watu 10 wamenitumia pesa, wameniambia wameona taarifa zangu katika gazeti la Mwanaspoti."
Ameongeza"Nashukuru gazeti la Mwanaspoti tangu nilipoumia limekuwa likinijulia hali na mmeandika taarifa ya maumivu yangu ambazo Watanzania wamejua bado sijapona na wamegugwa wameanza kunisaidia,maana sina kazi ninayofanya, kuna muda nilikuwa nakosa hata pesa ya chakula, nashukuru sasa angalau nitapata chakula."