Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbona Etoile wanafungika kiulaini tu

Ngassa akisumbua na beki wa Etoile ua Tunisia

Muktasari:

Wanaamini Yanga haiwezi kufanya maajabu ugenini na zaidi katika ardhi ya Waarabu ambao kwa muda mrefu klabu hiyo ya Tanzania haijawahi kutoka na ushindi

WADAU wengi wa soka walioshuhudia mchezo wa kwanza wa raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Yanga na Etoile du Sahel ya Tunisia Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, wamekata tamaa na kuamini Yanga imeshatolewa mashindanoni na Watunisia hao.

Wanaamini Yanga haiwezi kufanya maajabu ugenini na zaidi katika ardhi ya Waarabu ambao kwa muda mrefu klabu hiyo ya Tanzania haijawahi kutoka na ushindi.

Hali hiyo ya kukata tamaa imechagizwa zaidi na jinsi Etoile ilivyocheza kwa ustadi mkubwa katika mechi hiyo ya kwanza na kwa macho ya kawaida wadau haoa wanaamini kabisa kwamba hawawezi kwenda kuitoa Etoile nyumbani kwao.

Wengi tulikuwepo Taifa, nikiwamo mimi naitazama mechi inayokuja ikiwa haina mwenyewe, kwani timu yoyote kati ya Yanga na Etolie inaweza kusonga mbele na hapo chini nimejaribu kuanisha ambavyo Yanga ikifanya haya itapenya bila kutarajiwa.

Yanga haikuwa kwenye kiwango

Moja ya sababu kubwa iliyoifanya Etoile du Sahel ionekane kuwa bora kiasi cha kutia shaka mchezo ujao ni kwa vile, Yanga haikuwa kwenye ubora wake tuliouzoea. Yanga imekuwa ikionyesha ubora mkubwa inapocheza michezo yake ya Ligi Kuu ya Bara na kwenye mechi zao mbili za awali za Kombe la Shirikisho dhidi ya BDF XI ya Botswana na Platinum ya Zimbabwe.

Hata kama timu hizo hazikuwa na viwango vizuri kulinganisha na Etoile du Sahel, lakini ni lazima tukiri kuwa Yanga iliyocheza na Waarabu haikuwa ile iliyozoeleka. Haikucheza kabisa katika ubora wake na asilimia kubwa ya wachezaji wake hawakuwa bora katika mchezo ule.

Unaweza kuwahesabu wachezaji wanne au watano tu, waliokuwa kwenye kiwango kizuri akiwamo kipa Ally Mustafa ‘Bartez’, licha ya kufungwa bao linaonekana lilitokana na kutokuwa makini muda wote wa mchezo, bado aliisaidia sana Yanga kutofungwa.

Wengine ni Mbuyu Twite, Juma Abdul, Haruna Niyonzima pamoja na Mrisho Ngassa, wakati kina Oscar Joshua na Hassan Dilunga hawakuwapo kabisa uwanjani, hawakujipanga katika nafasi za kunyang’anya mipira, pasi zao zilienda upogo na hawakuwa na maamuzi ya haraka ya kuipunguzia Yanga idadi ya wachezaji.

Yanga hawakuwa wabishi

Ilionekana wazi wachezaji wa Yanga walikubali kunyanyaswa na Etoile du Sahel kwa kuwaacha wamiliki mipira muda mrefu, waliwaacha wapange mipango katikati ya uwanja. Yanga haikuwa makini kuhakikisha inakuwa ya kwanza kucheza mipira mirefu au pasi zinazopigwa kutoka golini kwa Etoile du Sahel.

Hata ilipotokea maamuzi ya utata, hawakuonyesha kushangazwa kama tunavyowaona wachezaji wa Ulaya na kwingineko wanavyofanya ikiwa ni haki ya wachezaji hasa nahodha kuhoji kwa marefa. Kwa mfano Yanga ilishindwa kuhoji kukataliwa kwa bao la Amissi Tambwe. Yanga ni tofauti na Simba inavyocheza dhidi ya timu za Kiarabu, watani hucheza bila urafiki, ule upole dhidi ya wachezaji wa Kiarabu haukupaswa, niliona kidogo kwa Yondani alipopishana kauli na mchezaji wa Etoile du Sahel, si vizuri kuwa hivyo, ila ukicheza na Waarabu unapaswa uwe na roho tofauti.

Ubora wa nguvu

Kulikuwa na tofauti kubwa katika matumizi ya nguvu uwanjani, wachezaji wa Etoile walikuwa bora sana pale ilipotokea hali ya kugombea mpira kwa mchezaji mmoja mmoja. Urefu wao na miili iliyojengeka iliwasaidia katika vita hiyo ya kugombea mpira mbele ya wachezaji wa Yanga.

Hata walipoamua kutembea na mipira ‘ku-dribble’ walitumia nguvu ya mikono kuwamzuia wachezaji waliowakaribia.

Kwa kifupi walikuwa bora kuanzia walivyojipanga kwa nidhamu kubwa. Kulikuwa na walinzi watano, viungo watatu na mbele kulikuwa na wachezaji wawili, mmoja mrefu akifanya kazi ya kupokea mipira yote ya juu iliyotoka nyuma na kumshushia mwenzake nadhani walikuwa kwenye mfumo wa 5:3:2.

Etoile du Sahel ilikuwa nzuri kutoka nyuma hadi katikati ya uwanja lakini haikuwa na mbinu nyingi katika ufungaji. Haikuonyesha hatari zaidi katika mipira ya adhabu ndogo, kona na mapigo mengine huru yaliyotokea uwanjani. Wachezaji wao si wanyumbulifu na wala hawakuwa na kasi kubwa kitu ambacho kingewasumbua mabeki wa Yanga ila walicheza kitimu.

Tatizo la maamuzi

Siyo siri moja kati ya vitu vilivyoitoa Yanga mchezoni uamuzi usio wa refa wa mchezo huo japo siyo rahisi kuona kwa macho kwamba waamuzi hawakuitendea haki timu mwenyeji.

Lakini waamuzi walikuwa hawatendi haki pale matukio yaliyooneka wazi kuelekea upande wa Etoile yalivyokuwa yakizimwa, kulikuwa na kutopigwa filimbi pale wachezaji wa Etoile walipo ruka kwa miguu miwili iliyonyooka pasipo mpira.

Vipo viashirio fulani pale mwamuzi alipotakiwa kuacha faida kwa mchezaji wa Yanga, badala yake alipiga filimbi unaweza kuona kama ni haki kwa filimbi kupigwa. Uhalisi alikuwa akiiwanyima kijanja Yanga nafasi ya kujenga mashambulizi ya moja kwa moja.

Sikuona tatizo katika bao lilikataliwa la Tambwe ambalo alifunga kwa mpira uliomkuta baada ya kumpita mchezaji wa Etoile du Sahel nyuma yake alikuwapo Tambwe.

Etoile inafungika kwao.

Kama wachezaji wa Yanga wataongeza umakini wa kulinda lango lao na kuongeza kasi ya mashambulizi ugenini na wakiwa na ubora wao wanaweza kupata bao la ugenini.

Yanga inaweza kutengeneza nafasi kama ilizozitengeneza Taifa na kitu kizuri ni kujaribu kuzitumia, isipotezea kama ilivyofanya katika mechi a kwanza.

Kama Yanga itaamua kupiga pasi za mwisho za chini, basi inaweza kumfikia mlinda mlango kirahisi na kufunga. Iwapo wachezaji wa Yanga wataamua kwa dhati kujituma na kuhakikisha wanakuwa wa kwanza kufika kwenye mipira yote itakayokuwa inadondokea kwenye eneo lao ili kutokubali wachezaji wa Etoile waanze kumiliki mchezo.

Mwalimu angalie uwezekano wa kuwatumia washambuliaji wawili. Imekuwa kawaida kwa Kocha Hans van de Pluijm kuwatumia mara kwa mara washambuliaji watatu Mrisho Ngassa, Msuva na Amissi Tambwe au Sherman huku viungo wakicheza Mbuyu Twite, Haruna Niyonzima na Salum Telela huku akiwa na walinzi wanne.

Mfumo huo umekuwa ukiipa uhai sana Yanga na hata mtiririko wa uchezaji wa Yanga umekuwa ukiendana na mfumo huo. Lakini kuelekea mchezo wa ugenini kuna haja ya kocha kuwa na viungo wawili wakabaji huku akiwatumia Haruna na Telela kuendesha timu ikitegemea pia na uzima wa wachezaji wote.

Kocha anaweza kuwatumia kwa pamoja Msuva na Ngassa ama Ngassa na Tambwe na vinginevyo, ingawa katika mfumo wowote ule ugenini itakuwa kazi kubwa iwapo atarudi katika kuwatumia washambuliaji watatu kwa pamoja na huku Andery Coutinho akiwa ndani kwani itamaanisha atakuwa na washambuliaji wanne kwani Mbrazil huyo si aina ya viungo wanaweza kushuka chini, kutembea na mipira.

Hivyo basi ,Yanga inaweza kuifunga Etoile iwapo itaamua na kujituma.