Mastaa Simba... Sakho anatisha nyie

MASTAA wa zamani walioacha heshima kubwa ndani ya Simba, wamewataka mashabiki wa klabu hiyo kuacha papara ya kupanikisha wachezaji, huku wakitolea mfano kwa straika Ousmane Sakho.
Wamesisitiza Sakho anatisha kwa sasa na punde atakuwa zaidi ya Clatous Chama na Luis Jose waliouzwa hivi karibuni Arabuni.
Sakho amezidi kung’aa baada ya kuuwasha moto kwenye Kombe la Mapinduzi huku akiiwezesha timu hiyo kutinga fainali na anatabiriwa kukinukisha zaidi kwenye fainali kesho.
Beki wa zamani Simba, Taifa Stars na Kilimanjaro Stars, Boniface Pawasa alisema lilikuwa suala la muda kwa Sakho kuonyesha kitu alichonacho licha ya mashabiki wengi awali kumbeza kwa kuangalia umbo na mwili wake.
“Niliwahi kusema awali ni suala la muda tu kwa Sakho kuonyesha kipaji chake, Watanzania huwa tuna kawaida  ya kutaka vitu vya haraka kwa wachezaji kitu ambacho tunakosea,” alisema Pawasa na kuongeza;
“Simba wakimvumilia  atakuwa zaidi ya Miquissone na Chama, mwanzo hakuzoea mazingira na aliumia kwenye mechi za mwanzo katika ligi lakini kwa sasa mechi mbili za Mapinduzi ameonyesha kitu.”
Pawasa aliongeza akisema;”Sakho ni mshambuliaji mzuri ambaye anawalazimisha wapinzani wafanye makosa, akishika mpira anawafuata mabeki na mguu wake unakuwa mwepesi nadhani akizidi kupewa muda atafanya makubwa zaidi.”
Naye mchezaji wa zamani Simba na Yanga, Zamoyoni Mogela alisema “Sakho ni mzuri na amethibitisha bila maneno bali vitendo vyake uwanjani, apewe muda naamini atafanya vitu vikubwa zaidi ya walivyofanya Chama na Luis.”
Sakho ameonyesha ubora kwenye kombe hilo akifunga mabao mawili katika mechi tatu alizocheza hali inayoonyesha yupo kwenye kiwango kikubwa kwa sasa.
Awali nyota huyu wakati anasajiliwa na Simba baada ya kuondoka mastaa wa kikosi hicho, Clatous Chama na Luis Miquissone alitafsiriwa na mashabiki kama hatoweza kuendana na kasi ya timu hiyo.
Sakho ambaye anazungumza Kifaransa kizuri na Kingereza kwa shida, alianza Ligi Kuu vibaya baada ya kuumia kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Dodoma Jiji na kumweka nje ya uwanja kwa muda mrefu, lakini baada ya kurejea anauwasha moto.
Urejeo wa mshambuliaji huyu unawaweka kwenye wakati mgumu Hassan Dilunga na Benard Morisson ambao mpaka sasa hawajawa chaguo la kwanza kwenye kikosi cha Simba Kombe la Mapinduzi.
Dilunga na Morisson kwenye ligi wameonyesha kiwango kizuri, huku  Morisson akijiweka pagumu zaidi kutokana na kukuta wenzake wameiva tangu arejee kutoka kwao Ghana alikokwenda kwenye tamasha lake.
Kazi imebaki kwa kocha wa Simba, Pablo Franco kuamua ni yupi aanze kwenye kikosi chake kwa sababu ni ngumu kumuona nje ya uwanja Sakho kwenye ligi huku akiwa ameshachanganya.