Luis na Chama hadi raha yaani

Muktasari:

  • MASTAA wawili wa Simba, Luis Miquissone na Larry Bwalya wamefunguka walivyonogewa kimataifa.

MASTAA wawili wa Simba, Luis Miquissone na Larry Bwalya wamefunguka walivyonogewa kimataifa.

Miquissone mwenye mabao matatu katika hatua ya makundi alisema Simba ni timu kubwa si kutokana na jina bali mambo ambayo wanayafanya.

“Ukiangalia wachezaji wa Simba pamoja na benchi la ufundi mara nyingi hatujali tunacheza na wapinzani wa namna gani, tunakuwa na mbinu zetu za nyumbani na ugenini ambazo ndio zimetufanikisha kutupa matokeo haya mazuri mpaka sasa,” alisema mchezaji huyo mwenye thamani kubwa kwa sasa ndani ya Simba.

“Hatukuwa na mechi rahisi tangu tulivyoaanza safari ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika lakini malengo ambayo benchi la ufundi walitupatia pamoja na wachezaji kila mmoja kutimiza majukumu yake yametufanikisha kufika hapa,” alisema.

“Bado tuna kazi ngumu zaidi mbele yetu kwani mashindano haya kadri ambavyo yanazidi kwenda mbele ugumu unaongezeka kutokana na aina ya timu ambazo zimebaki zinakuwa bora zaidi ila tupo tayari kwa hilo na nina imani tutafanya vizuri na kufikia malengo ambayo tulijiwekea kabla ya msimu kuanza.

“Tumebakiwa na mechi ngumu moja katika hatua hii ambayo tutacheza dhidi ya Al Ahly ugenini. Kikubwa mechi hiyo nayo tunatamani kupata matokeo mazuri licha ya kujihakikishia kumaliza katika nafasi ya kwanza kwenye kundi letu,” alisema Miquissone.

“Simba inafanya vizuri na inafuatiliwa na timu nyingi kwa maana hiyo lazima wachezaji wake nikiwamo mimi kuhusishwa kwenda kujiunga na klabu nyingine lakini nadhani Mwanaspoti mnafahmu kila kitu, bado nipo na mkataba wa miaka miwili na timu hii kwahiyo kabla ya timu yoyote kunitaka wanatakiwa kuzungumza na uongozi,” aliongezea Miquissone.

Kwa upande wa Bwalya alisema; “Mechi ya Al Ahly ni ya kukamilisha ratiba lakini hawatakubali kupoteza mara mbili dhidi yetu kama ambavyo nasi hatutapenda kuona tunaharibu rekodi ya kupoteza katika hatua hii.”

“Aina ya timu zilizobaki pengine ni bora kuliko ambazo zilizotoka kwahiyo ugumu na changamoto ambayo tunakwenda kukutana nayo ni kubwa zaidi.

“Unajua unapomaliza nafasi ya kwanza katika kundi ambalo lina Al Ahly unazifanya timu nyingine kukukamia zaidi,” alisema Bwalya.