Lionel Messi abeba tuzo ya nne Ulaya
Muktasari:
Safari hii hakuwa mwenye kupata tabu katika hotuba yake, tofauti na ilivyokuwa mwaka uliopita wakati ambao hakuwa na matarajio ya kushinda, hakuwa ameandika chochote lakini alifikiri kile ambacho alitaka kukisema, hakuhitaji kuweweseka kwa namna yoyote ile.
TOLEO lililopita Mwandishi Luca Caioli alielezea namna Messi alivyoweka rekodi kwa kutwaa tuzo ya tatu ya Ballon d’Or na kuingia katika orodha ya kihistoria ya mastaa wengine wa soka Ulaya waliofanya hivyo kabla yake. Endelea…
Kwa tuzo yake ya tatu mfululizo akawa ameungana kwa tuzo hiyo na kina Michel Platini (1983, 1984, 1985) Johan Cruyff (1971, 1972, 1974) na Marco Van Basten (1988, 1989, 1992) akaingia kwenye kundi la heshima ya kihistoria. Lakini hakuna aliyepiga ‘hat trick’ (tuzo tatu) kama hiyo akiwa na miaka 24.
Katika mchuano wa tuzo hiyo nyuma ya Messi alikuwa Ronaldo na Xavi akaibuka wa tatu.
Mara tu baada ya kusikia jina lake, Messi alimkumbatia Xavi aliyekuwa amekaa pembeni yake katika ukumbi wa mikutano jijini Zurich kisha akaelekea jukwaani.
Kama kawaida yake alikuwa amepiga suti ya Dolce & Gabbana huku shingoni akiwa ‘amejinyonga kwa’ tai nyeusi, alionekana kuwa katika hali ya utulivu tofauti na ilivyokuwa mwaka uliopita, siku ambayo hali ya furaha isiyo kifani ilimtawala.
Safari hii hakuwa mwenye kupata tabu katika hotuba yake, tofauti na ilivyokuwa mwaka uliopita wakati ambao hakuwa na matarajio ya kushinda, hakuwa ameandika chochote lakini alifikiri kile ambacho alitaka kukisema, hakuhitaji kuweweseka kwa namna yoyote ile.
Baada ya kuwashukuru wapigakura, wachezaji wenzake wa Barca na kikosi cha Argentina, Messi alibakisha shukrani za kipekee kwa kumtaja namba 6 wa Barca.
“Hii ni muhimu napenda kumshirikisha tuzo hii ya Ballon d’Or rafiki yangu Xavi,’’ alisema Messi. “Hii mara ya nne tumeshiriki hafla ya tuzo hii pamoja, nawe pia una haki ya kupata tuzo hii, ni jambo zuri kuwa pamoja nawe hapa pamoja na uwanjani.”
Akiwa tayari amebeba tuzo yake, Messi alisema baada ya hafla ya tuzo hiyo: “Sikuwahi kuota kwamba ningeweza kushinda tuzo hii mara mbili, achilia mbali mara tatu, namaanisha hili ni jambo la kipekee na heshima, ingawa nisingeweza kufanikisha lolote katika haya bila ya kuwa na wachezaji wenzangu, watu wangu wa nguvu.”
“Na ndio maana tuzo hii ni heshima kwa Xavi, naamini tutaweza kuendelea kuwa nayo kwa miaka mingine ijayo ingawa nayo ni changamoto, jambo la muhimu ni kuendelea kudumisha ubora wetu wa sasa.
Ronaldo hakuwapo katika hafla ya tuzo hiyo kwani Real Madrid ilikuwa na mechi ya Kombe la Mfalme dhidi ya Malaga siku iliyofuata.
Ronaldo ndiye aliyempeleka Xavi hadi nafasi ya tatu kwa kupata asilimia 9.23 wakati Ronaldo aliyekuwa nafasi ya pili alipata asilimia 21.6 wakati Messi alipata asilimia 47.88.
Kwa upande mwingine matokeo ya kura hizo maana yake ni kwamba Ronaldo alifanikiwa kurudi kwenye tatu bora baada ya kukosekana kwenye nafasi hiyo kwa mwaka mmoja.
Ni kielelezo tosha cha mabao yake 40 ya kwenye La Liga ambayo yalimpa tuzo ya kiatu cha dhahabu Ulaya na kuisaidia Real kutwaa Kombe la Mfalme kwa kuibwaga Barca katika fainali, lakini hakuwa wa kumfunika Messi.
Mafanikio mengi yalikuwa mbele ya Mess, ni kama Platini alivyowahi kusema, Messi ni mchezaji muuaji, yuko imara na atafanikisha mengi, bado kijana tunatakiwa tumuache asafirie kipaji chake kabla ya kujua wapi ataishia.
“Sijui labda atanipita mimi lakini ukweli ni kwamba bado ana miaka mingi ya kucheza soka na ataendelea kushinda mambo mengi.”
Akizungumzia mambo yake ya baadaye Messi alisema, “Nitakuwa mwenye furaha na kutosumbuka na mambo ya Ballon d’Or kwa miaka miwili ijayo kama Argentina itashinda taji la dunia, kushinda Kombe la Dunia litakuwa jambo la kipekee, hiyo itamaanisha sisi ni mabingwa wa dunia, hilo litakuwa jambo kubwa kuliko.
Hata hivyo, alirudi tena kwenye Ballon d’Or mwaka uliofuata na kuweka historia ya kuwa mchezaji pekee kutwaa tuzo hiyo mara nne licha ya kukiri haukuwa mwaka mzuri kwake. Alitwaa taji moja pekee mwaka 2012, Kombe la Mfalme ingawa Oktoba 29 aliweka rekodi alipobeba kiatu cha dhahabu kwa mara ya pili akiwa mfungaji mwenye mabao mengi katika ligi za Ulaya kwa msimu wa 2011/12 akitwaa pointi 100 huku Ronaldo akiwa wa pili kwa pointi 92 na Van Persie wa Arsenal alishika nafasi ya tatu kwa pointi 60.
Itaendelea Jumamosi ijayo…