LaLiga yajitosa michuano ya Chipkizi Cup

Mkurugenzi wa Future star Alfred Itael Kushoto ambao ndio waandaji wa mashindano hayo ya Chipkizi Cup, wakisalimiana na mjumbe Kutoka LaLiga, Jorge Gazapo baada ya mazungumzo ya namna ya kuboresha Mashindano hayo yalete tija Kwa vijana hasa kucheza soka la kulipwa nje ya nchi

Zaidi ya timu 220 za soka la vijana Kutoka nchi mbalimbali zimethibitisha kushiriki michuano ya Kombe la Chipkizi Afrika Mashariki msimu wa 13 inayotarajiwa kufanyika jijini Arusha, Desemba 13-18 mwaka huu.

Michuano hiyo iliyoandaliwa na taasisi ya kuibua na kukuza vipaji cha Future Stars Academy yenye makao yake makuu jijini Arusha, awamu hii inaungwa mkono na Ligi Kuu ya Hispania (LaLiga) huku ikizikutanisha timu kutoka nchi 10 za Afrika na duniani.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Future Stars Academy, Alfred Itaeli alisema mashindano hayo ya Afrika Mashariki yanayojulikana kama 'Chipkiz cup' yamemevutia zaidi ya timu 200 kutoka nchi za Falme za Kiarabu, Marekani, Somalia, Cameroon, Zimbabwe na Nigeria ambao watashiriki Kwa mara ya kwanza.

" Timu Kutoka nchi hizo zimeshathibitisha kushiriki na wanasubiri ratiba pekee ya kuja kushindana ambazo zitaungana na timu wenyeji za Afrika mashariki Kutoka Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Zanzibar na Tanzania bara"

Alisema maandalizi yote kuelekea mashindano hayo yamekamilika, huku wakimalizia kukarabati viwanja watakavyotumia ikiwemo Sheikh Amri Abeid na za shule za kimataifa zilizoko Arusha ambapo mashindano yatashirikisha timu za vijana chini ya umri wa miaka saba, tisa, 11, 13, 15, 17, 20 na wasichana chini ya miaka 11, 15 na 20.


Naye Mjumbe wa Maendeleo ya Kimataifa kutoka LaLiga,  Jorge Gazapo alisema ni furaha kwa LaLiga kushiriki katika kombe la Chipkizi ambapo wanatarajia kuleta baadhi ya makocha kutoka timu za vijana kuja kuvuna vijana watakaoonesha kiwango kizuri Kwa ajili ya kuwaendeleza.


"Kujitolea kwa LaLiga hadi mashinani hakuna shaka, ndiyo sababu kwa sasa tupo Arusha kwani tunaamini kwamba mustakabali wa uendelevu wa soka uko kwa vijana hivyo ushirikiano huu tumeanza kwenye mashindano haya kwa ajili ya kuwapa vijana wa Tanzania uwanja mpana wa kucheza soka la kulipwa nje kupitia chipkizi cup," alisema.
Kwa Upande wake katibu wa chama Cha soma mkoa wa Arusha, Emmanuel Anthony alisema kuwa watashirikiana na waandaji kuhakikisha Mashindano yanafanikiwa Kwa manufaa ya soka la Arusha na taifa kwa ujumla.