Kocha Ruvu aanza visingizio

KOCHA Mkuu wa Ruvu Shooting, Khalid Adam amesema sababu kubwa iliyochangia kuanza vibaya kwenye Ligi ya Championship msimu huu ni kutokana na kuchelewa kuanza maandalizi tangu timu hiyo ilipohamishiwa Iringa.

Adam aliyekabidhiwa timu hiyo msimu huu baada ya kuachana na KMC, alisema licha ya maandalizi duni ila kuna mwelekeo mzuri mbeleni.

“Tulikuwa na siku 10 za maandalizi kabla ya kuanza kwa msimu sasa utaona ni kwa jinsi gani mambo yalivyokuwa magumu, ligi ni ngumu sana na licha ya mwanzo mbaya ila bado safari ni ndefu na hatujakata tamaa,” alisema.

Aidha aliongeza jambo kubwa analolifanyia kazi ni kutengeneza muunganiko wa wachezaji.

Timu hiyo iliyoshuka daraja msimu uliopita na sasa inamilikiwa na manispaa ya mkoani Iringa ambapo taratibu kwa ajili ya kuibadilisha jina zinaendelea na pindi tu zitakapokamilika itakuwa ikifahamika kama Lipuli FC.

Ruvu ilianza na kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya FGA Talents kisha ikapoteza bao 1-0 na Polisi Tanzania.

Ruvu ilikuwa timu ya kwanza kushuka Ligi Kuu  msimu iliopita ikafuatiwa na Polisi Tanzania na baadaye ikafuata Mbeya City baada ya KMC kunusurika.