Kocha Mlandege ‘achimba’ mkwara ZPL, anaitaka nne bora
Muktasari:
- Mlandege jana Jumamosi ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Zimamoto na kufikisha pointi 40 baada ya mechi 24, zikibaki sita kumaliza msimu huu.
KOCHA Msaidizi wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), Mlandege, Sabri China amesema ushiriki wao katika Kombe la Muungano umekuwa kipimo kizuri kwa timu hiyo na imerudi kwenye ubora wake kama awali.
Mlandege ni kati ya timu zilizoiwakilisha Zanzibar katika mashindano hayo pamoja na KVZ, Muembe Makumbi na Mafunzo zilizoishia robo fainali, huku yenyewe ikifika nusu fainali.
Kocha huyo alisema kitendo cha kufika hatua hiyo kimeonyesha ubora walionao na mipango yao msimu huu ni kumaliza nafasi nne za juu endapo watashindwa kutetea taji lao.
Sabri alisema mipango na mikakati imerudi na itakuwa ni aibu kwa timu hiyo iliyotwaa ubingwa msimu uliopita 2024/25, kumaliza ligi nje ya nne bora.
"Haiwezekani timu ichukue ubingwa wa ligi kisha imalize bila ya kufika nafasi ya nne bora msimu unaofuata, tunahitaji nafasi hiyo," alisema.
Alisema kwa sasa wanahamasisha wachezaji kuendeleza walipoishia Kombe la Muungano kwani nafasi ipo na uwezo wanao.
Mlandege jana Jumamosi ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Zimamoto na kufikisha pointi 40 baada ya mechi 24, zikibaki sita kumaliza msimu huu.