KMC yaipiga mkwara Yanga

Friday April 09 2021
KMC pic
By Mwandishi Wetu

KIKOSI cha KMC kinaendelea kujifua kwa ajili ya mchezao wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga huku mabosi wao wakisisitiza wamejiandaa kuwadhalilisha vinara hao na mabingwa wa kihistoria wa ligi hiyo.


KMC inatarajiwa kuwa wageni wa Yanga katika mchezo huo wa marudiano, ikiwa na kumbukumbu ya kucharazwa mabao 2-1 jijini Mwanza, lakini ikitambia rekodi yao walipokutana mara ya mwisho jijini Dar es Salaam kwa kuwacharaza wapinzani wao kwa bao 1-0.


Mchezo huo wa wikiendi huu utachezwa saa 1:00 usiku kwenye Uwanja was Benjamin Mkapa, huku Yanga ikiwa kileleni na alama zao 50 kutokana na michezo 23, huku wapinzani wao wakicheza mechi 24 na kukusanya alama 35.


Kocha Mkuu wa KMC, John Simkoko amesema vijana wake wapo tayari kwa vita hiyo ya pointi tatu, kiu yao ni kupata ushindi katika mchezo huo ili kujiimarisha katika msimamo licha ya kukiri anatarajia kupata upinzani mkubwa toka kwa wenyeji wao.


“Tunakwenda kwenye mchezo ambao kimsingi hautakuwa mwepesi kutokana na aina ya timu tunayokutana nayo, ni nzuri, wanafanya vizuri, pia wanaongoza ligi, hivyo mchezo utakuwa mgumu lakini bado KMC tutapambana kupata alama tatu na tunaimani kubwa ya kufanya vizuri," amesema.

Advertisement