Kiwango kilipanda, Ronaldo akaenda Ureno na Messi akatua Hispania
Muktasari:
- Linapokuja suala la klabu sifa zao zinatofautiana, Ronaldo amecheza katika klabu tatu Sporting Lisbon, Man United na Real Madrid (ya nne Juventus) wakati Messi ameishia katika klabu moja, Barcelona.
KATIKA toleo lililopita mwandishi, Luca Caioli alituonyesha safari ya Messi ilivyokuwa kabla ya kumgeukia Ronaldo na kuchambua matukio ya mwanzo mwanzo ya soka la ushindani. Sasa endelea…
“Wakati akiwa katika uwanja wa soka wa Shule ya Malvinas, kipa alimpasia mpira akiwa eneo la ulinzi, akakimbia nao eneo lote la uwanja hadi kwenda kufunga goli zuri, hakuhitaji kufundishwa kitu, nini ungemfundisha Maradona au Pele? Ni mambo madogo mno kwa kocha kuyaweka sawa.”
Hadi hapo kilichobaki ni kuanza safari ya kuvuka ‘bwawa’ kuelekea bara Ulaya ambako Cristiano Ronaldo alianza kwa kujiunga na Sporting Lisbon na Messi safari yake ikaanzia FC Barcelona.
Linapokuja suala la klabu sifa zao zinatofautiana, Ronaldo amecheza katika klabu tatu Sporting Lisbon, Man United na Real Madrid (ya nne Juventus) wakati Messi ameishia katika klabu moja, Barcelona.
Sifa hizo zinaweza kuonekana ni kitu kidogo lakini ukweli ni kwamba zina umuhimu wake. Je Messi angeweza kuendana na mazingira kama angekumbana na hali tofauti tofauti katika vyumba vya kubadilishia nguo?
Vipi Ronaldo naye hulka anazohusishwa nazo za kujiona yuko juu ikidaiwa ndio maana amecheza katika klabu tatu (sasa nne) za mataifa tofauti.
Hapana shaka kwamba safari ya kila mmoja wao, ina maana kubwa katika hatua waliyofikia na mafanikio waliyoyapata hadi wakati huu. Hebu tuangalie hatua hizo.
Msimu wa 2003/03
Sporting ni nyumbani kwa Cristiano Ronaldo, pamemtengeneza hadi kufikia hatua aliyofikia sasa, klabu hii ya Lisbon ilimpa nafasi ya kwanza yenye maana kubwa na kumuwezesha kung’ara na ikamuandaa kuondoka alipokuwa tayari kuwa staa.
Julai Mosi, 2002, hatua ambayo Cristiano Ronaldo alikuwa akiisubiri kwa hamu hatimaye ilifikia, alipokuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza.
Alikuwa akipewa sapoti na kocha Mromania, Laszlo Boloni, kiungo wa zamani wa Steaua Bucharest ambayo iliifunga Barcelona katika michuano ya Ulaya mwaka 1986.
Ronaldo alianza kung’ara akiwa katika mechi za awali za maandalizi ya msimu na kocha wake akamfanyia mabadiliko madogo ya hapa na pale. Ronaldo wakati huo alipenda kucheza mbele na kocha wake akaamua kumhamishia kwenye winga ya kushoto.
Kocha Boloni alichotaka kufanya ni kutumia kasi yake vizuri lakini pia ilikuwa vizuri kwa sababu wakati huo bado hakuwa na nguvu za kukabiliana na mabeki wa timu pinzani.
Hakumwangusha, alikuwa mwenye kasi, mahiri kumiliki mipira na kutoa dalili zote za kuwa tishio, “Huyu kijana wa kuangalia, ‘’ liliandika gazeti la michezo nchini Ureno la Record.
“Alikuwa akijua namna ya kuwaacha vibaya wapinzani wake, aliweza kupiga chenga na alijua ‘kunusa vyema’ goli.”
Na kijana huyo anayezungumzwa alikuwa na mengi ya kusema baada ya mechi ya kujiandaa na msimu dhidi ya Paris Saint German. “Wadau bado hawajamuona Ronaldo mwenyewe, huu ni mwanzo tu.’’
Alionyesha kujiamini na asiye na woga, alikuwa mwenye uhakika katika jambo lake, hapo ndio kwanza alikuwa kijana wa miaka 17.
Agosti 14, 2002, alicheza mechi yake ya kwanza ya ushindani, dhidi ya timu ya Inter Milan ya Italia katika mechi za awali za Ligiya Mabingwa Ulaya. Hakukuwa na kipa lakini kiwango chake cha ubora ni dhahiri kilijionyesha na kuacha alama.
Hata hivyo, hapo hapo kukawa na ukosoaji, alikuwa akikimbia mno peke yake na kuwa tayari kwa makabiliano ya ana kwa ana, ni mtazamo na hamasa za kitoto, ni jambo ambalo angejisahihisha baada ya miaka michache.
Ni wazi kwamba alikuwa mwenye uwezo wa kulifurahisha jukwaa, na alidhihirisha hilo katika mechi mbili za nje, Oktoba 7 katika mechi ya Ligi Kuu Ureno, wakati huo vinara walikuwa ni Moreirense FC ambao ndio kwanza walikuwa wamepanda daraja.
Itaendelea Jumamosi ijayo…