Kitambi ampunguzia presha Lusajo

KOCHA wa Namungo, Denis Kitambi amemwambia straika wake, Reliants Lusajo; “Acha presha. Cheza mpira.” Staa huyo anapitia kipindi kigumu cha kutofunga ambapo Kitambi amemtaka kutosikiliza maneno ya watu.

Kitambi ambaye ni miongoni mwa wasomi wazawa, ameliambia Mwanasoti kuwa anatambua furaha ya mshambuliaji siku zote ni kuona anafunga ila kukaa muda mrefu kwake isimfanye kujisikia vibaya na kushindwa kutimiza majukumu yake vizuri akiwa uwanjani.

“Ni kweli ana muda mrefu lakini suala hilo humtokea mchezaji yoyote, siwezi kusema nimuweka benchi eti tu kwa sababu ya maneno ya watu isipokuwa nitaendelea kumchezesha kama njia ya kumjenga,” alisema na kuongeza:

“Watu wanatakiwa kuangalia kutokufunga kwake anatengenezewa nafasi vizuri na viungo? sasa ukiangalia katika kikosi changu hilo ndilo jambo tunalolifanyia kazi kuhakikisha kila mmoja anatimiza majukumu yake vizuri.”

Lusajo ambaye ana mabao sita hadi sasa amekuwa na ukata wa kutupia tangu mara ya mwisho alipoifunga Mbeya City Novemba 4, mwaka jana.

Akizungumzia mchezo wao wa Jumanne na KMC, Kitambi alisema kila mchezaji yupo kwenye hali nzuri na baada ya kupoteza mabao 2-0 dhidi ya Polisi Tanzania wanahitaji pointi tatu zitakazowarejesha katika ushindani.

“Tunaenda kucheza na timu ngumu lakini sisi kama benchi la ufundi tunaamini tumefanyia kazi mapungufu yote yaliyotokea katika mchezo uliopita na matarajio yetu ni kuona tunapata matokeo chanya,” alisema Kitambi.

Katika mechi saba zilizopita baina ya timu hizi kwenye Ligi Kuu Bara Namungo imeshinda moja tu na kupoteza miwili huku minne iliyobaki ikiisha kwa sare na mara ya mwisho kukutana zilitoka suluhu Oktoba Mosi mwaka jana.