KIBANDA UMIZA: Simba kuwalipia Yanga viingilio

MASHABIKI wa Simba wa kibanda umiza cha Dos Santos Arena kilichopo Tabata Kimanga wameahidi kuwalipia viingilio mashabiki wa Yanga katika mechi zote za Simba za Kombe la Shirikisho Afrika.

Hii ni kufuatia mwenendo mzuri wa Simba katika Kombe la Shirikisho ambapo Jumapili iliyopita walifanikiwa kuvuna alama moja mbele ya US Gendamarine kisha kukaa kileleni mwa kundi D na pointi nne wakifuatiwa na Asec Mimosas na RS Berkane wenye pointi tatu kila mmoja.

Jambo hilo lilitamkwa na shabiki maarufu mitaa hiyo wa klabu hiyo baada ya mchezo kumalizika huku akiwaomba mashabiki wenzake wa Simba kuwalipia viingilio wale wa Yanga michezo ijayo ya kimataifa. Mmiliki wa kibanda umiza hicho, Kathbeti alisema kuwa utani uliopo baina ya mashabaki wa timu hizo kongwe nchini ni mkubwa mno jambo ambalo limemfanya kuweka mpaka wa mashabiki hao wanapokuwa kwenye kibanda hicho - upande mmoja wanakaa Yanga na mwingine Simba.