KANU : Atapeliwa mabilioni ya fedha kwao Nigeria
Muktasari:
- Washtakiwa hao inasemekana walichota pesa hizo za hoteli ya Kanu wakitumia kisingizio cha kufanya matengenezo katika hoteli ya Kanu ikiwa ni pamoja na kutanua ukubwa wa hoteli hiyo na kuzinakshi upya nyumba na vyumba pamoja na chumba cha mikutano cha hoteli hiyo.
LAGOS,NIGERIA
NWANKWO Kanu ametafuta pesa zake kwa shida maishani. Wakati mwingine alihatarisha maisha yake uwanjani kwa kucheza huku akiwa na matatizo ya ugonjwa wa moyo. Lakini sasa ametulia na utajiri wake huku wengine wakijaribu kuuchota kwa kumtapeli.
Kanu ametapeliwa kiasi cha dola 9 milioni za Marekani kupitia kwa hoteli yake ya jijini Lagos kwao Nigeria na tayari mtu mmoja ametiwa ndani kwa kosa hilo.
Mkurugenzi Mkuu wa Hardley Suites Hotel jijini Lagos, Ayoola Gam Ikon, 49, ametiwa ndani na kushtakiwa kwa kosa hilo la utapeli wa mamilioni ya fedha dhidi ya staa huyo wa zamani wa Arsenal.
Timu ya wapelelezi wa Polisi imemtia ndani Ikon, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Hardley Suites Limited iliyopo mtaa wa Elsie Femi Pearse jijini Lagos kwa kile kilichotajwa kumuibia Kanu kiasi hicho cha pesa.
Mwingine aliyetiwa ndani katika kesi hiyo ni mfanyakazi wa Hoteli ya Kanu, Oke Samuel na walipelekwa katika mahakama ya Igbosere wakituhumiwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Polisi walikiri kwamba Ikon na mwenzake wameshtakiwa na Kanu pamoja na mkewe, Ogbonna Kanu kwa wizi uliotokea kati ya mwaka 2005 na 2012. Washtakiwa hao inasemekana walichota pesa hizo za hoteli ya Kanu wakitumia kisingizio cha kufanya matengenezo katika hoteli ya Kanu ikiwa ni pamoja na kutanua ukubwa wa hoteli hiyo na kuzinakshi upya nyumba na vyumba pamoja na chumba cha mikutano cha hoteli hiyo.
Hata hivyo, inasemekana Ikon na Oke hawakutumia pesa hizo kwa matumizi hayo na badala yake wakazigeuzia katika matanuzi yao binafsi.
Ikon alikwenda mbali zaidi kwa kuitumia Hoteli hiyo ya Kanu kwa ajili ya kupata mkopo wa mamilioni ya pesa kutoka katika benki ya Skye bank Plc bila ya ruhusa ya Kanu na bodi ya hoteli yake.
Hata hivyo washtakiwa hao wawili walikana mashtaka hayo ingawa mwendesha mashtaka alitaka waendelee kusota rumande kwa sababu mahakama hiyo haikuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo kwa mujibu wa sheria za Nigeria.
Hata hivyo, Hakimu mkazi, O.O Oshin alikataa wazo hilo akinukuu vifungu kadhaa vya mashtaka hayo kabla ya kuongeza kuwa mahakama hiyo ilikuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo. Baadaye aliwaachia kwa dhamana washtakiwa hao.
Kanu ni miongoni mwa wachezaji matajiri nchini Nigeria na ambaye amekuwa akiheshimiwa na jamii ya watu wa Nigeria kutokana na mchango wake mkubwa alioutoa ndani na nje ya uwanja nchini humo.
Achilia mbali kumiliki hoteli hiyo, Kanu anamiliki duka kubwa la picha katika mtaa maarufu wa Allen Avenue uliopo jijini Lagos huku pia akitajwa kuwa na nyumba tatu za kifahari katika eneo la kitajiri la Park View, Ikoyi.
Achilia mbali utajiri huo, Kanu pia anajihusisha katika biashara ya mafuta ambayo ni miongoni mwa biashara maarufu nchini Nigeria huku akishirikiana na wafanyabiashara kadhaa maarufu.
Kanu, ambaye ni mzaliwa wa Jimbo la Owerri, Imo pia amekuwa akijihusisha katika biashara ya upngajishaji wa nyumba zake pamoja na Hospitali.
Anapendwa zaidi na watu wa Nigeria kwa moyo wake wa kujitolea katika jamii yake na haikushangaza wakati alipochaguliwa kuwa Balozi wa Shirika la Umoja la Mataifa la Unicef kwa miaka miwili mfululizo.
Kabla ya kujikita vema katika soka la kulipwa anajulikana kwa tatizo lake la ugonjwa wa moyo ambalo nusura likwamishe ndoto zake za kuwa mwanasoka wa kulipwa. Hata hivyo baadaye alifanyiwa operesheni nchini Marekani ambayo ilimuwezesha kucheza soka la uhakika.
Kutokana na kupona huko, alijikuta akitumia muda wake mwingi kusaidia watoto maskini wa Afrika ambao wana matatizo ya ugonjwa wa moyo. Kwanza alianza kusapoti mfuko wa Heart of Gold Hospice na baadaye kufungua mfuko wake mwenyewe wa Kanu Nwankwo Heart Foundation ambao umelenga katika kusaidia watoto wasio na uwezo ambao wanashambuliwa na ugonjwa wa moyo.
Wengi wamekuwa wakitibiwa ndani nan je ya Nigeria na kwa sasa wamekuwa wakiishi maisha bora tofauti na awali.
Katika soka alitwaa medali ya dhahabu na Nigeria mwaka 1996 nchini Marekani huku akishiriki Kombe la Dunia mwaka 1998 na 2002. Alichana na soka la kimataifa Juni 24, 2010 baada ya Nigeria kutolewa katika hatua ya makundi nchini Afrika Kusini.
Aliichezea nchi yake mechi 86 na kufunga mabao 13 tu huku kwa wakati huo akiwa mchezaji aliyeichezea nchi hiyo mechi nyingi kando ya Muda Lawal. Kwa sasa rekodi hiyo inashikiliwa na Joseph Yobo.