Kally apewa mikoba Azam FC

UONGOZI wa Azam FC umefikia makubaliano ya kumkabidhi timu aliyekuwa kaimu kocha mkuu, Kally Ongala hadi mwisho wa msimu.

Uamuzi huo umefikiwa kutokana na kiwango bora ambacho timu hiyo imekuwa ikikionyesha chini yake, hivyo viongozi wa juu wameamua kusitisha taratibu za kutafuta kocha mpya licha ya wengi kujitokeza kuwania nafasi hiyo.

Akizungumza na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam, Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Abdulkarim Amin ‘Popat’ alisema mwenendo mzuri wa kikosi hicho ndio sababu ya kuamua kumpa timu Kally kwani amerejesha heshima kikosini.

“Ametengeneza heshima na umoja kwa wachezaji na hicho ndicho kitu kikubwa ambacho tumeona amefanikiwa kwa sababu ili timu yoyote ipate matokeo mazuri ni lazima hayo mambo yote yawepo,” alisema Popat na kuongeza;

“Hatuna mpango tena wa kutafuta kocha mwingine hivyo ataendelea kusalia hadi mwisho wa msimu, sisi kama viongozi tutahakikisha tunamuunga mkono huku tukitimiza matwaka yote ya wachezaji na benchi lake la ufundi.”

Kwa upande wa Kally alisema ni heshima kubwa kuendelea kuaminiwa huku akisisitiza licha ya kufanya vizuri ila bado shauku yake ni kurejesha heshima ya klabu hiyo na kutoa dhana iliyojengeka kwa watu ya kuonekana wa kawaida.

Alichukua nafasi hiyo baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu Mfaransa, Denis Lavagne aliyeteuliwa Septemba 7 na kutimuliwa Oktoba 22 kutokana na kiwango kibovu cha timu hali iliyosababisha kuondolewa Kombe la Shirikisho Afrika.

Kally amekiongoza kikosi hicho michezo sita ya Ligi Kuu na kushinda yote akianza na ushindi wa (1-0) v Simba, (1-0) v Ihefu, (2-1) v Dodoma Jiji, (4-3) v Mtibwa Sugar, (1-0) v Ruvu Shooting na (1-0) v Namungo.