KAH! YANGA SASA BASI : yazichonganisha Simba na Azam, Mzimbabwe akubali kutua

Mashabiki wa Yanga wakishangilia timu yao ilipoitandika timu ya Ruvu Shooting 5-0. Picha na Said Khamis
Muktasari:
Vinara hao waliobakiza pointi tatu tu kutangazwa kuwa mabingwa wapya, walipata ushindi huo kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na kuwafanya wafikishe jumla ya pointi 52.
YANGA ni kama imeshafunga hesabu za msimu wa ligi Kuu Bara 2014-2015 baada ya jana Ijumaa jioni kuendeleza wimbi lake la ushindi katika Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuichapa Ruvu Shooting mabao 5-0.
Vinara hao waliobakiza pointi tatu tu kutangazwa kuwa mabingwa wapya, walipata ushindi huo kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na kuwafanya wafikishe jumla ya pointi 52.
Pointi hizo zinaweza kufikiwa na Azam pekee yake ambayo ina pointi 42 na leo Jumamosi itashuka uwanjani kupepetana na Stand United katika mfululizo wa mechi za ligi hiyo. Katika pambano la jana, Simon Msuva alifunga mara mbili na kufikisha jumla ya mabao 16, huku mfungaji bora wa msimu uliopita, Amissi Tambwe alifikisha bao lake la 11 msimu huu. Yanga walianza pambano hilo kwa kasi na kuwachukua dakika 14 kuandika bao la kuongoza lililotumbukizwa kimiani na Msuva akiunganisha kwa kichwa mpira wa faulo uliopigwa na Amissi Tambwe. Faulo hiyo ilitokana na yeye Msuva kuchezewa vibaya na mabeki wa Ruvu.
Wakati maafande wa Ruvu wakitafuna njia ya kurejesha bao hilo, Mliberia Kpah Sherman aliandika bao la pili ya Yanga akimalizia mpira wa kona ndefu iliyopigwa na Msuva.
Maafande hao waliolazimisha sare ya 0-0 katika mechi ya duru la kwanza, walijaribu kusaka bao la kufutia machozi na kufanya kosa kosa nyingi kabla ya kushtuliwa kwa bao la tatu lililofungwa sekunde chache kabla ya mapumziko lililowekwa nyavuni na Msuva tena aliyeunganisha kwa kichwa krosi pasi ya Haruna Niyonzima.
Kipindi cha pili kilianza kwa Ruvu kufanya mabadiliko ya wachezaji, lakini haikuwasaidia kuizuia Yanga, kwani Amissi Tambwe aliiandikia Yanga bao la nne katika dakika ya 57 kwa juhudi binafsi baada ya kuwatoka mabeki wa Ruvu kabla ya kumhadaa kipa Abdallah Rashid.
Sherman aliwathibitishia mashabiki kuwa sasa amerudi kwenye kiwango chake kwa kuandika bao la tano la Yanga katika dakika ya 67 kwa kuunganisha kichwa krosi ya Juma Abdul. Hilo likiwa ni bao lake la pili kwa jana na la nne msimu huu. Mpaka filimbi ya mwisho ya mchezo huo, Yanga walikuwa wababe kwa maafande wa Ruvu.
YANGA;
Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Oscar Joshua/Edward Charles, Rajab Zahir, Kelvin Yondani, Said Juma, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Mrisho Ngassa na Kpah Sherman/Hussen Javu
RUVU;
Abdallah Rashid, Michael Aidan, Abdul Mpambika, George Assey, Hamis Seleman, Salvatory Ntebe, Raphael Kyala/Juma Nade, Ally Khan, Yahya Tumbo, Baraka Mtuwi/ Juma Mpakala na Abdulrahman Mussa/Mwita John.