Job asaini miwili Yanga
Muktasari:
- Mwanaspoti linajua beki huyo kisiki alikuwa na mazungumzo ya kimyakimya na Simba na Azam wakati mkataba wake ukiwa ukingoni, jambo lililowatia presha mashabiki wa Yanga kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Job akiunda ukuta wa chuma Jangwani akishirikiana na na mabeki wengine tangu aliposajiliwa.
HUENDA taarifa hii isiwe njema kwa timu zilizokuwa zikimpigia hesabu Dickson Job, kwani beki huyo wa kati wa Yanga amekata mzizi wa fitina kwa kusaini mkataba mpya wa miaka miwili utakaomuweka Jangwani hadi 2025.
Mwanaspoti linajua beki huyo kisiki alikuwa na mazungumzo ya kimyakimya na Simba na Azam wakati mkataba wake ukiwa ukingoni, jambo lililowatia presha mashabiki wa Yanga kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Job akiunda ukuta wa chuma Jangwani akishirikiana na na mabeki wengine tangu aliposajiliwa.
Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema, Job amesaini mkataba huo juzi mchana baada ya kukubaliana na viongozi juu ya fedha alizokuwa akizitaka ukiwamo mshahara wa Sh10 milioni na huenda wakamtangaza muda wowote.
Awali ilielezwa beki huyo na jopo linalomsimamia waligomea dau alilowekewa mezani sambamba na kiwango cha mashahara aliokuwa akitaka kulipwa na Yanga iliotaka kumpa Sh4-6 milioni akikomalia Sh10 milioni.
Hata hivyo baada ya pande mbili kukaa chini na kukubaliana, waliafikia mambo yasiwe mengi na uongozi kukubali kulipa kile alichotaka beki huyo wa kimataifa aliyeibuliwa na Mtibwa Sugar.
Hakuna kiongozi aliyethibitisha taarifa hizi kwa kilichoelezwa wapo bize na maandalizi ya mechi ya Kariakoo Derby, itakayopigwa kesho kwenye Kwa Mkapa, lakini mtu wa karibu wa mchezaji huyo alithibitisha kuwa kila kitu kimeenda sawa na Job ni mali ya Yanga hadi 2025.