Jina la Msenegal mezani kwa Ibenge
Muktasari:
- Nyota huyo alijiunga na Shabana FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya katika dirisha dogo la Januari 2026, kwa mkopo hadi mwishoni mwa msimu wa 2025-2026, baada ya kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza cha Azam FC.
WINGA wa Azam FC raia wa Senegal, Pape Doudou Diallo amerejea tena ndani ya kikosi hicho baada ya mkataba wake wa mkopo na Shabana FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya kumalizika, huku hatima yake ikibakia mikononi mwa Kocha, Florent Ibenge.
Nyota huyo alijiunga na Shabana FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya katika dirisha dogo la Januari 2026, kwa mkopo hadi mwishoni mwa msimu wa 2025-2026, baada ya kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza cha Azam FC.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu Msaidizi wa Azam, Rashid Seif amesemalengo la kumtoa mchezaji huyo kwa mkopo kwenda Shabana FC ni kwa ajili ya kumpatia nafasi zaidi ya kucheza, kutokana na ushindani wa namba kikosini humo.
“Bado ana mkataba na kumtoa kwetu kwa mkopo haina maana sio mchezaji mzuri isipokuwa tulihitaji kumpatia timu itakayompa nafasi zaidi ya kucheza hasa kikosi cha kwanza, baada ya kurudi benchi la ufundi litaamua hatima yake,” amesemaRashid.
Diallo aliyejiunga na kikosi hicho cha Azam FC Julai 30, 2025, akitokea ASC La Linguere de Saint-Louis aliyoichezea kwa mkopo kutokea Generation Foot, msimu wa 2024-2025, aliibuka mfungaji bora wa Ligi ya Senegal baada ya kufunga mabao 11.
Nyota huyo anayeweza kucheza wingi zote ya kulia na kushoto huku akicheza pia nyuma ya mshambuliaji kwa ufasaha, amekosa nafasi ya kuonekana zaidi katika kikosi hicho cha Azam, jambo lililowafanya pia mabosi wa timu hiyo kumuachia akacheze.
Usajili wa Mzee Hassan Mzee ‘Aziz KI’, aliyejiunga na kikosi hicho katika dirisha dogo la Januari 2026, akitokea KMKM ya visiwani Zanzibar, kumechangia kwa kiasi kikubwa pia nyota huyo kutolewa kwa mkopo, ili akapate nafasi sehemu nyingine.
Nyota huyo aliyezaliwa Desemba 26, 2002, ana mkataba na Azam hadi Juni 30, 2027, ambapo alijiunga na Shabana iliyomaliza Ligi Kuu ya Kenya msimu wa 2025-2026, ikiwa nafasi ya tano na pointi 52, baada ya kushinda mechi 14, sare 10 na kupoteza 10.