Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ivo Mapunda : Ishu yake na Eto'o iko hivi unaambiwa -2

Muktasari:

Pia, nyota huyo aligusia mataulo aliyokuwa akiyatumia kujifuta wakati wa mechi kuhusishwa na ushirikina. Leo anahitimisha suala hilo na ushauri wake katika soka. Endelea..

Katika sehemu ya kwanza ya makala haya, kipa mstaafu wa timu mbalimbali nchini, nje na ile ya taifa ‘Taifa stars’, Ivo Mapunda alizungumzia mambo mbalimbali ikiwamo maisha yake ndani ya Simba na Yanga, Stars na uamuzi alioufikia hivi karibuni kwenda kuombewa kanisani baada ya pingili za mgongo kuanza kumsumbua.

Pia, nyota huyo aligusia mataulo aliyokuwa akiyatumia kujifuta wakati wa mechi kuhusishwa na ushirikina. Leo anahitimisha suala hilo na ushauri wake katika soka. Endelea..

“Nilipogundua kwamba (wapinzani wetu) wametishika na taulo niliona hiyo ndio njia sahihi ya kupata ushindi kwa timu yangu, maana mataulo yaliwaharibu kisaikolojia, hivyo kila nikiingia naingia nalo, hapo si wachezaji wala mashabiki walikuwa na hofu na kweli wakawa wanapoteza mechi,” anasema.

“Baadaye niliitwa na kampuni moja hivi ya kimataifa nayo nadhani iliona ni njia ya kutangaza biashara yao, walinitengenezea taulo nyingi sana ambapo kila mechi niliingia na taulo zaidi ya tano ambazo ziliandikwa jina la kampuni hiyo.

“Hivyo nikiingia wakilalamika kwa mwamuzi akilitoa (taulo) napewa lingine ama wakati mwingine nawarushia mashabiki na wao wanafurahia wakidhani yana kitu cha ajabu kumbe ni nguo tu kama zinavyouzwa sehemu nyingine.”

Ivo anasema hakuhofia kelele za kuambiwa anatumia ushirikina kwenye taulo zake kwani ukweli aliufahamu mwenyewe.

“Ndiyo maana hata kocha wangu wakati nipo Gor Mahia alinitumia sana kwenye mechi za kuamua matokeo na kwa vile nilijua udhaifu wao (wapinzani), basi tulipata matokeo mazuri kirahisi kupitia taulo langu lililowatisha na kuwatoa mchezoni wachezaji wa timu pinzani,” anasema.

“Gor Mahia sikuwa kipa namba moja ila nilikuwa kwenye kiwango kizuri, nilifurahia kuanzia benchi kwani nilijua umuhimu wangu ndani ya timu. Hata nilipotua Simba niliingia kwa staili ileile ya kutumia taulo na kwa vile walikuwa wamesikia habari za taulo hata hapa walianza kuwa na hofu juu yangu.

“Kuna mechi yetu na Yanga nilinyang’anywa taulo na wachezaji wa Yanga walilirusha kwa mashabiki, lilichanwachanwa lakini baadaye kocha wangu Logarusic ambaye pia alikuwa na tabia ya kuingia na taulo alinipa lake, walivurugwa sana hata baada ya kuwafunga bao walivamia goli kulitoa lile taulo nililopewa.

“Huku na huko walisawazisha bao hilo, hapo ndipo waliamini wamesawazisha kwa sababu walifanikiwa kulitoa taulo langu, kumbe ni jitihada zangu tu. Hivyo wadau wa soka waamini kwamba hakuna nguvu ya ushirikina inayofanya kazi kwenye soka, bali mafanikio yanakuja kwa jitihada za wachezaji na mbinu za makocha pekee.”

Umeme’ wa Yanga

Katika mechi ya Simba na Yanga iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, Ivo akiwa kipa wa Wanajangwani alijikuta ‘akila umeme’ wa miezi sita na Shadrack Nsajigwa.

Adhabu hiyo ilikuja baada ya kuhisiwa na viongozi wao kuwa waliihujumu timu kwa kupokea pesa kutoka Simba ili wafungwe katika mechi kati ya timu hizo.

Simba ilipata bao kupitia kiungo wao Ulimboka Mwakingwe ambaye alimpiga chenga Nsajigwa, kisha kufunga bao hilo lililoleta tafrani ndani ya Yanga.

“Halikuwa jambo rahisi kwangu na sikuwahi kulitarajia kwenye maisha yangu kama lingetokea, lakini baadaye nilitambua kuwa tukio hilo lilitoka kwa nia ya kunikomaza kiakili, shida ya hizi timu zina mihemko hakuna upande unakuwa tayari kupokea matokeo mabaya,” anasema.

Sh10 milioni za Simba

Baada ya kutoka Gor Mahia, Ivo alisaini mkataba wa mwaka mmoja na Simba, na ulipomalizika baadhi ya viongozi walitaka kumpa mwingine huku wengine wakigoma, hivyo alibaki katikati.

Anasema, “niliambiwa nani hahitaji niongezwe mkataba, ila walikuwa wamenipa Sh10 milioni kama kishika uchumba cha kusaini mkataba mwingine, tulikubaliana kila kitu ambapo waliniambia wangenipigia simu ili nikamwage wino, hivyo nilikuwa nawasikilizia wao tu.

“Baadaye nilisikia kwenye vyombo vya habari kwamba sipatikani mara sitaki kwenda kusaini, ndipo nilipowafuata viongozi kuwaulizia hii ishu ikoje mbona nipo na nawasubiri wao, nilijibiwa kwamba kikao kimeamua tuachane na wewe.

“Waliniuliza kuhusu pesa yao niliwaeleza wazi kuwa ilipoingia tu niliingiiza kwenye biashara zangu, hivyo nitailipa mara baada ya biashara yangu kukaa sawa, hivyo hadi muda huu biashara yangu kwa kweli haijakaa sawa.

“Hiyo ndiyo ilikuwa sababu ya kwenda Azam kwani huku tayari dili lilishindikana na Azam walikuwa wakinihitaji, hakukuwa na kitu kingine wao ndio hawakutaka huduma yangu - tena watu wachache tu.”

Eto’o kumjengea uwanja

Nyota wa zamani, Barcelona na timu ya taifa ya Cameroon, Samuel Eto’o ni miongoni mwa rafiki wa Ivo, baada ya wote kujikuta wakiwa ni mabalozi wa Castle Five Africa, ambapo kwenye urafiki wao huo mlinda lango huyo ameahidiwa kupata sapoti kwenye ujenzi wa uwanja wake wa michezo.

“Eto’o anafahamu vyema matatizo ya soka la Afrika, katika stori za hapa na pale tukafikia suala la kunisaidia kujenga uwanja, aliniambia nitafute sehemu ya wazi, nimeipata hivyo taratibu zote zikikamilika nitamtaarifu ili aone ni namna gani atanisaidia kwenye ujenzi huo,” anasema.

Aipa neno TFF

Ivo analishauri Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwekeza kwenye vituo vya soka au kuwaunga mkono wenye vituo kwa nia ya kujenga msingi imara wa wachezaji ambao watalitumikia Taifa.

“Tupo wengi wenye vituo hivi vya kukuza vipaji vya watoto, ni vyema TFF wangeweka ubia nasi ili kuongeza nguvu ya vituo, hivyo kuwa imara zaidi, tungekuwa tunaandaa wachezaji wa kucheza timu zetu za Taifa.

“Lakini ni tatizo kama TFF inakosa mpango wa muda mrefu, kwa mfano baada ya miaka mitano kufanya kitu kikubwa cha kisoka ambacho kitakuwa na matokeo ya misingi mizuri na siyo kufanya mambo kwa kubahatisha.”

Mafanikio, familia

Ivo anasema amepata mafanikio mengi kupitia soka kwani hiyo ndiyo ilikuwa ajira yake kubwa. “Sijawahi kuwa na ajira nyingine zaidi ya soka, soka limenipa mafanikio makubwa, naishi kwangu na nina maeneo mengine ambayo nimeyapata kupitia soka, ndiyo maana hata sasa namiliki hiki kituo cha michezo, yote hayo ni matunda ya kucheza mpira,” anasema.

Kipa huyo mstaafu mwenye umri wa miaka 48 amechezea timu 10 ambazo ni Tukuyu Stars, Prisons, Moro United, Yanga, St George ya Ethiopia, African Lyon, Bandari FC ya Mombasa, Gor Mahia ya Nairobi, Simba na Azam FC.

Ivo ni baba wa familia yenye watoto wanne anaowataja kwa majina ya Prince (17), Yvonne (11), Ignasia (5) na Nyanchimbi (4).

“Naipenda sana familia yangu japokuwa mke wangu anaishi mkoani kwa sababu anafanya kazi huko, huyu wa kwanza anamaliza kidato cha nne na ndiye anayependa soka hasa nafasi kama niliyokuwa natumikia mimi (golikipa),” anasema Mapunda na kuongeza:

“..na huwa anacheza huko shuleni na kwenye mashindano mbalimbali ya kishule akiwa kama kipa.”