Ishu ya Ulimwengu na Yanga iko hivi
KATIKA soka la Tanzania kwenye kizazi cha sasa majina makubwa ni Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu. Hilo halina ubishi.
Ndio Watanzania wa kwanza kucheza Fainali za Kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika walipokuwa na TP Mazembe mwaka 2016 na kutwaa taji hilo.
Hata hivyo, baada ya hapo, kila mmoja aliangalia usawa wake katika kusaka maisha mapya ya soka. Samatta akatimkia Ubelgiji katika klabu ya KRC Genk na Ulimwengu haikujulikana alipokwenda. Mwenyewe anaelezea ilivyokuwa,
“Unajua wakati namalizia mkataba Mazembe ilikuja ofa ya Saint Ettiene ile ya Ufaransa, ilileta barua lakini sikuweza kwenda kwa sababu ya majeraha ya goti, yalinifelisha mambo mengi, ikabidi sasa kuingia jukumu la kujitibia mwenyewe majeraha yangu.
“Niliuliza kwa wachezaji wenzangu sehemu gani sahihi ambayo nitapata tiba ya goti langu na nikaambiwa Afrika kusini, Capetown na ilinibidi niende kule na yote hiyo ni katika kupambania afya yangu,” anasimulia.
“Nilifika kule pia sina ndugu kwa hiyo ikabidi nichukue nyumba na nilipofanyiwa upasuaji nikamchukua rafiki yangu kutoka Dar ili aje akae na mimi na kunisaidia vitu vidogo vidogo kwa sababu nilikuwa natakiwa kufanya mazoezi na kupumzika kuliko kitu kingine, ujue nilikuwa najigharimia,” anasema na baadae alienda Italia katika Hospital ya Isokinetic.
“Nilitoka Sauzi nikapita Ubeligiji kwa Samatta nikakaa pale na kufanya mazoezi kidogo kisha nikaenda Italia, kile kituo kilikuwa na wachezaji wengi wa ligi za pale ambao walikuwa wanakuja kwa ajili ya kliniki.”
AFICHUA KILICHOMwONDOA JS SAOURA
“Unajua pale tulikuwa weusi kama wawili hivi, kuna vitu vilikuwepo pale sio vizuri kuvizungumzia, nikaomba kuondoka bosi akawa hataki.”
Alisema licha ya bosi wa klabu hiyo kugoma, alipata ofa ya AS Vita na walikuwa tayari kutoa Dola 150,000, lakini bado walikuwa hawataki kumwacha.
“Walitaka Dola 150000 na As Vita walipofika na dau hilo jamaa wakapandisha, As Vita wakaweka lakini bado wakawa hawataki niondoke,” alisema Ulimwengu na kuongeza kuondoka klabu hapo ilibidi suala lake liende Fifa na ndipo akashinda kesi ya kuachana na klabu hiyo.
“Unajua nilirudi na kukaa nyumbani bila timu lakini vuta nikuvute yangu na Js Saoura ilikuwa inaendelea na nilishinda kesi yangu, nawadai pesa zangu nyingi JS Saoura mpaka kesho ni kiasi kikubwa sana kiukweli.”
KATUMBI AMREJESHA MAZEMBE
“Baada ya kutoka fainali za Afcon kule ndio ikaja ofa ya Mazembe, Horoya na sehemu nyingine, niliwekewa ofa nzuri zaidi ya Mazembe lakini niliamua kurudi nyumbani baada ya kuongea na bosi Katumbi.
“Bado nina safari ya kucheza Ulaya na ninaamini katika hilo, mipango ipo nilisaini mkataba wa miaka miwili na mpaka hivi sasa nimemaliza mwaka kwa hiyo nimebakiza mmoja, lolote litatokea,” alisema.
AWAZIMIA SIMU YANGA
Anasema wakati anaanza kupewa mzuka na wazungu kuhusu kucheza soka la kulipwa Ulaya, alijikuta akichomoa ofa za Simba na Yanga licha ya kuwekewa pesa nyingi.
Anasema Simba walimuwekea Sh20 milioni na Yanga walimuwekea 25 milioni, lakini aliamua kupotezea ofa zote.
“Ilikuwa nusu nisaini Yanga kwa milioni 25 kwa kipindi hicho, lakini usiku wa kuamkia kwenda kusaini nilipokea simu ya Damas Ndumbaro kuna dili la kwenda Sweden.
“Baada ya kukutana nae nilizungumza na wale wazungu basi ikabidi nizime kabisa simu ili Yanga wasinipate na baada ya hapo nikatimka zangu Sweden huku nikiwa na akili hata nikiwa naenda kucheza bure ni sawa tu kwangu,” anasema huku akifichua baba yake mzazi alikuwa hapendi acheze soka.
Ulimwengu anasema Kocha Lubala wa Area C Dodoma alimtaka pia akacheze katika timu hiyo ya mtaani na ndipo safari ya soka ikawa inaanzia hapo.
Ulimwengu anasimulia mwaka 2008 kulikuwa na mashindano ya vijana chini ya miaka 17 (Copa Cocacola) alipata bahati ya kuja na timu hiyo mkoani Dar es Salaam.
“Nakumbuka walikuwa pia wanatafuta wachezaji wa timu ya vijana, nikiwa Dar sikumbuki tulicheza na nani ile mechi lakini nakumbuka nilifunga mabao matatu na hapohapo Kipingu aliniita na kuniandika jina.”
BOLTON WONDERERS
Baada ya kuondoka jijini Dar es Salaam huku akiwa kichwa chini baada ya kutoswa katika timu ya Vijana, Ulimwengu alirejea mkoani Dodoma na timu yake huku akiendelea kupambania ndoto zake.
Ghafla ilikuja klabu ya Bolton Wonderers nchini kwa lengo la kutengeneza Akademi na walikuwa wakipita mikoa mbalimbali na hapo Thomas Ulimwengu alibahatika kuchaguliwa na kuja tena jijini Dar es Salaam.
“Dodoma tulitoka vijana watatu lakini tulipokuja Dar tulikuwa wengi, ukafanyika mchujo tukabaki 25 na mimi nipo hapo.
“Hapo ilikuwa wachezaji wa mikoa yote tunachuana, ilikuwa wakati mgumu lakini niliamua kupambana kuweza kutimiza ndoto yangu ya kucheza tu mpira.”
Ulimwengu anasema kupitia wazungu hao ambao walifungua kituo cha Tanzania Soccer Academy (TSA) hapa nchini mara kwa mara walikuwa wanaelezwa lengo kubwa ni kucheza Ulaya.
“Tulikuwa tunapelekwa katika timu za Ligi Kuu ili kupata uzoefu, mimi nilicheza Moro United, sikusaini mkataba hapo wao TFF ndio walitusaidia sisi kupata nafasi,” anasema akaenda Sweden.
Alipofika Sweden; “Nikakaa kidogo ikabidi nitafute wakala Ufaransa ili niende kwenye akademi ya Monaco lakini bado ilishindikana kwa sababu nao walikuwa wanataka vigezo.”
Aliongeza kwa kusema baada ya mipango yote kushindikana basi akawa anakaa katika akademi na kufanya mazoezi pamoja na kucheza mechi ndogondogo kutokana na kibali cha kazi alikosa.
APELEKWA MAZEMBE MAJARIBIO
Baada ya kushindwa kucheza soka la kulipwa Ulaya kutokana na kuwa chini ya miaka 18, basi wazungu walifikiria kumtafutia timu Afrika.
Ulimwengu anasema ilimlazimu kurejea tena Afrika lakini moja kwa moja alienda Mazembe kwenda kupambania nafasi ya kucheza soka la kulipwa.
“Mazembe ujue ndio nikakutana na Kalaba ambaye alikuwa ametoka kucheza sijui Kombe la Dunia, Mputu akiwa kwenye ubora wake wa hali ya juu lakini nilikuwa nasema hapa napambana kupata nafasi kwa sababu Ulaya nimeshafeli.
“Nilipewa mechi ya kirafiki, ndipo mwalimu akasema ananihitaji kwa ajili ya baadae kwa sababu Mazembe huwa wana kikosi cha sasa lakini na cha baadae ambacho huwa kinatengenezwa taratibu,” anasema.
Mwaka 2010 alienda Hamburg Sv ambayo ilikuwa na nyota kama Rud Van Nistelrooy lakini akakwama kutokana na majeraha na ugumu wa kupata vibali akarudi tena Mazembe.
Baada ya dili lake kufeli pale Hamburg basi mwaka 2011 aliamua kusaini mkataba wa miaka mitano kuitumikia TP Mazembe, klabu ambayo ni tishio barani Afrika.
Ulimwengu akiwa na klabu hiyo alibeba makombe mbalimbali ya Ligi pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na Mbwana Samatta.
AKUMBUSHIA UGUMU ITALIA
Ulimwengu anasema wakati akiwa anajitibia alikuwa haangalii ni kiasi gani cha pesa ambacho anatumia katika kuhakikisha anapona, kwani aliamini pesa ataipata pale atakapoanza kucheza.
“Ndugu yangu maisha ya Italia pale achana nayo, mambo ya nyumba kwanza, ukija tu katika mizunguko yako ya siku lazima utumia Dola 150 (laki tatu na elfu arobaini na sita) lakini ilikuwa haina namna kwa sababu natafuta uhai wa mguu wangu.”
“Uzuri madaktari wa pale ni wazuri sana tena sana, waliona nimekatika Ligament za ndani ambazo zinashikilia goti kwa hiyo baada ya matibabu wakawa wananifanyisha mazoezi wao wenyewe, mnacheza mechi kabisa na kuangalia kama upo fiti au bado haujawa fiti,” amesema na kuongeza akiwa hospitalini alipata dili ya Bosnia lakini hakuwa na namna.
“Nilipata dili katika klabu ya FK Sloboda wakati hapo sijacheza popote ujue halafu nimetoka kwenye majeraha, nilifika kule kama leo halafu kesho kuna mechi.
“Uzuri mwalimu wa ile timu alikuwa anajua mazingira yangu ya majeraha kwa hiyo aliniambia kabisa atanipa dakika 45 za kucheza na nilicheza na ndipo taratibu za kusajiliwa zilipoanza.”
Ulimwengu huku akicheka alisema; “Unajua nchi za wenzetu zina mambo mengi sana, mimi nilisaini mpaka mkataba na Sloboda (2017), lakini waliponiomba cheti cha Diploma tu ilibidi niondoke kwa sababu mimi niliishia kidato cha nne.
“Mkataba ule ulikuwa ni wenye thamani ya Dola 150000, pesa nzuri ilikuwa kwa kiasi chake ukiangalia nilikuwa sijacheza muda mrefu, lakini sikukata tamaa,” anasema na kuongeza ndipo akapokea simu ya Al-Hilal ya Sudan wakati akijiandaa kurudi Bongo.
“Nilipigiwa simu na wakala mmoja anaitwa Camara nahitajika Sudan nikamwambia ndio kwanza nipo uwanja wa ndege narudi nyumbani, akaniambia jamaa hawana muda hivyo natakiwa nifike Tanzania na kuondoka na mimi nilifanya hivyo, nikasaini mwaka mmoja nikaenda Algeria.”
ALGERIA
Sudan alisani mkataba wa miaka miwili katika klabu hiyo lakini aliichezea kwa msimu mmoja tu baada ya hapo aliomba kuondoka.
“Nilipata pesa nzuri na nikiwa pale nilifunga mabao 13 kwa msimu mmoja katika ligi, nilikuwa na kipindi kizuri licha ya kwamba ndio nilikua naanza kuwa fiti kwa kupata muda wa kucheza.
“Pale niliondoka kwa sababu kuna mambo yalitokea ambayo siwezi kuyasema, lakini nashukuru uongozi na mimi tulikubaliana na kuachana bila taabu yoyote.
Mwaka 2019 aliibukia Js Soura kwa mkataba wa miaka miwili lakini napo alikaa kwa mwaka mmoja kisha akawa hajulikani alipo mpaka alipokuja kuibukia Mazembe.