Huyu hapa mchezaji bora Ligi Kuu Tanzania 2021/22

IKIWA imesalia michezo michache kabla ya pazia la Ligi Kuu Bara kufungwa kitendawili kilichobaki ni nani ataibuka mchezaji bora wa msimu.

Kuna nyota wanaotajwa huenda wakatwaa tuzo hiyo ambayo msimu uliopita alitwaa kiungo fundi wa Simba, Clatous Chama kabla ya kwenda RS Berkane ya Morocco.

Nyota hawa wamekuwa na mchango mkubwa kwenye vikosi vyao na mwisho wa msimu tuzo hii mmoja lazima aipate.


DJIGUI DIARRA

Diarra amekuwa kipenzi cha mashabiki wa Yanga kutokana na ubora wake. Anaweza kuwa mchezaji bora wa msimu kulingana na takwimu zake kwani hajaruhusu nyavu zake kuguswa kwenye michezo 15.

Raia huyo wa Mali ameifanya Yanga kuwa kwenye mikono salama, amempiga bao kipa wa Simba, Aishi Manula ambaye kwa zaidi ya misimu minne amekuwa akitesa. Manula hajaruhusu nyavu zake kuguswa kwenye michezo 11.


FISTON MAYELE

Kwa moto aliouonyesha Yanga, Mayele ana nafasi ya kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa msimu. Kwa kiasi kikubwa mabao yake yamewasaidia Wananchi kutwaa ubingwa wa ligi baada ya ukame wa msimu minne.

Nyota huyo wa kimataifa wa DR Congo, anapambana na George Mpole kuwania kiatu cha ufungaji bora, wawili hao wote wana mabao 16.


HENOCK INONGA

Inonga ana nafasi ya kuwa mchezaji bora wa msimu wa Ligi Kuu Bara na hakuna shaka amejipambanua sana hasa kwa upande wa michuano ya kimataifa ambao waliishia hatua ya robo fainali Kombe la Shirikisho. Simba ilitolewa na Orlando Pirates ya Afrika Kusin kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya kutoka sare kwa matokeo ya jumla 1-1.


GEORGE MPOLE

Mshambuliaji huyo wa Geita Gold ameonyesha uwezo wa kufunga mabao ya kawaida, pia anaweza kufunga kwa mipira ya kutenga.

Akaunti ya Mpole ina mabao 16 huku akitoa asisti nne. Bila shaka hiki ni kilele cha ubora wake na anaweza kuwa mchezaji bora wa msimu.


YANNICK BANGALA

Ni kiraka ambaye ameifanya Yanga kuwa na uhai kwenye maeneo mawili tofauti ambayo yote amekuwa akitoa ubora wa namna yake, kuna kipindi alikuwa akicheza kama beki wa kati sambamba na Dickson Job au Bakari Mwamnyeto na hata kiungo mkabaji.

Hakuna ubishi Bangala ni mmoja wa wachezaji wa kigeni bora kabisa kucheza Ligi Kuu Bara, mchango wake ni mkubwa kwenye ubingwa ambao Yanga imetwaa hivyo ana nafasi ya kuwa mchezaji bora wa msimu kulingana na nidhamu yake na kiwango alichokionyesha msimu huu.