Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hamtuwezi au bado mnabisha!

YANGA imeshindikana. Vinara hao wa Ligi Kuu Bara usiku wa jana waliendeleza rekodi yao ya kutopoteza mchezo, baada ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi 2021 kwa kuwanyoosha watani wao, Simba kwa penalti 4-3, huku mashabiki wa timu hiyo wakiwatambia wenzao kwa kuiimba hamtuwezi...hamtuwezi...!

Pambano hilo lililopigwa kwenye Uwanja wa Amaan, visiwani hapa lilimaliza dakika 90 kwa timu hizo bila kufungana huku mashabiki wakiikosa ile burudani iliyozoeleka kwa Kariakoo Derby, kutokana na wachezaji kucheza ovyo.

Huo ulikuwa ushindi wa kwanza kwa Yanga dhidi ya Simba katika michuano hiyo na likiwa taji lao la pili baada ya lile ililotwaa mwaka 2007 baada ya mshambuliaji, Saido Ntibazonkiza aliyeitwa kikosini akiamua mchezo huo kwa kupiga penalti ya mwisho iliyoipa ushindi.

Mara ya mwisho kwa Yanga kupoteza mechi ilikuwa Machi 12, mwaka jana walipofungwa bao 1-0 na KMC na baada ya hapo imecheza mechi 34 za mashindano bila kupoteza ikiwamo 30 ya Ligi Kuu na nne za Kombe la Mapinduzi ambao waliruhusu bao moja hadi wanabeba kombe.

Shujaa wa Yanga, Saido akizungumza mara baada ya mchezo huo, alisema japo hakuwa fiti kwa asilimia zote, lakini alipambana na kushukuru kufunga mkwaju uliowapa ubingwa.

Katika upigaji wa penalti, nahodha wa Simba katika mchezo huo, Meddie Kagere na Joash Onyango walikosa mikwaju yao, huku kwa upande wa Yanga Mukoko Tonombe naye alipoteza mkwaju wake uliotolewa na kipa Beno Kakolanya.

Tuisila Kisinda, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Zawadi Mauya na Saido ndio waliokwamisha nyavuni mikwaju ya Yanga, huku Francis Kahata aliyekuwa Mchezaji Bora wa michuano hiyo, Chriss Mugalu na Gadiel Michael wakiwamisha kwa upande wa Msimbazi.

Katika dakika 90 za mchezo huo ambao mgeni rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar, Dk Hassan Mwinyi, ulianza kwa kasi na dakika ya sita tu Miraji Athuman wa Simba alikosa bao akiwa amepiga shuti kali lililogonga mwamba na kutoka nje huku dakika tatu baadaye Saido akipiga mpira uliompata Michael Sarpong aliyepaisha juu. Safu ya ushambuliaji ya Yanga ilionekana kutokuwa makini katika umaliziaji kwani, Sarpong aliinyima tena timu yake bao dakika ya 25 baada ya kupiga mpira uliookolewa na kipa wa Simba, Beno Kakolanya baada ya mabeki wake kupoteza umakini wa kulinda hatari hiyo.

Mwamuzi wa mchezo huo, Nassir Salum Siahi alitoa kadi za njano kwa wachezaji watatu akianza na David Kameta ‘Duchu’ baada ya kucheza rafu na dakika ya 28 Haruna Niyonzima wa Yanga naye akipewa kadi dakika ya 32 kwa kumchezea rafu Yassin Mzamiru huku kadi ya mwisho ya kipindi cha kwanza ikienda kwa Kennedy Juma wa Simba aliyemchezea rafu Kisinda.

Simba walikosa bao dakika ya 38 baada ya Kahata kupiga mpira wa kona uliompata Onyango aliyepiga kichwa na kutoka nje kidogo ya goli huku Sarpong akipoteza tena bahati dakika ya 38 baada ya kupiga shuti nje akipokea pasi nzuri ya Kisinda.

Makocha wote wawili walifanya mabadiliko kipindi cha pili ambapo Cedric Kaze wa Yanga aliwatoa Adeyun Salehe/Paul Godfrey, Sarpong/Waziri Junior wakati Seleman Matola aliwatoa Hassan Dilunga aliyapata maumivu ya paja nafasi yake ilichukuliwa na Chris Mugali, Miraji akimpisha Ibrahimu Ajibu.

Katika kipindi hicho cha pili Niyonzima alipiga shuti kali akipokea krosi ya Kisinda, lakini lilidakwa na Kakolanya huku Saido akipiga mpira wa faulo dakika ya 54 baada ya Kisinda kuchezewa rafu. Ajibu naye alipaisha mpira akipiga shuti lililopita juu ya lango la wapinzani ikiwa ni dakika ya 90.

Beki Mkenya wa Simba, Onyango alichaguliwa Nyota wa mchezo huo na kuzoa Sh 1 milioni akifikisha idadi ya wachezaji bora watatu kwa mechi tofauti kutoka Simba akianza na Miraji pamoja na Kahata.

Miraji pia ndiye alikuwa kinara wa mabao katika mashindano hayo akifunga mara nne, wakati kipa wa Yanga, Shikhalo alichaguliwa Kipa Bora huku Yanga wakilamba Kombe, medali na Sh 15 milioni, huku Simba walinyakua Sh 10 milioni.

YANGA: Farouk Shikhalo, Kibwana Shomari, Adeyun Salehe, Said Makapu, Abdallah Shaibu, Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda, Zawadi Mauya, Michael Sarpong, Said Ntibanzonkiza na Haruna Niyonzima.

SIMBA: Beno Kakolanya, David Kameta, Gadiel Michael, Kennedy Juma, Joash Onyango, Tadeo Lwanga, Hassan Dilunga, Mzamiru Yassin, Meddie Kagere, Francis Kahata na Miraji Athuman.