Gofu vijana mguu saw michuano ya Afrika
Wachezaji watimu ya Taifa ya gofu ya vijana wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa mchezo huo hapa nchini. PICHA | MAJUTO OMARY
Muktasari:
- Timu hiyo itajumuisha jumla ya wachezaji nane na viongozi watano kwa mujibu wa mwenyekiti wa chama cha gofu Tanzania (TGU), Gilman kasiga.
Dar es Salaam. Timu ya Taifa ya gofu ya wachezaji vijana wa Tanzania inatarajia kuondoka nchini Aprili 15 kuelekea Kampala, Uganda kushiriki mashindano ya Afrika.
Timu hiyo itajumuisha jumla ya wachezaji nane na viongozi watano kwa mujibu wa mwenyekiti wa chama cha gofu Tanzania (TGU), Gilman kasiga.
Kasiga aliwataja wachezaji hao kuwa ni Shufaa Twalib, Sabrina Likuli na Juliana Kowaku ambao wanatashiriki kwa upande wa wasichana huku wavulana ni Ibrahim Gabriel, Aliabbas Kermali, Karim Abdallah na Ramadhani Matinga.
Msafara huo utawajumuisha makocha Athuman Chiundu kwa upande wa wanaume na Madina Idd kwa upande wa wanawake.
Mkuu wa msafara kwa mujibu wa Kasiga ni Danstan Kolimba ambapo viongozi wengine ni Maryanne Mugo na Naftali Ayonga.
Kasiga alisema kuwa ushiriki wa timu hiyo katika mashindano hayo umetokana na msaada mkubwa kutoka kwa benki ya NCBA, kampuni ya bima ya Stategis na balozi wa India nchini Binaya Pradhan.
Alisema kuwa kwa sasa wachezaji hao wapo katika mazoezi makali kwenye uwanja wa Lugalo na baadaye watahamia Arusha kabla ya kuondoka nchini.
Mashhindano ya Afrika yanashirisha jumla ya nchi 17 ikiwemo Tanzania. Nchi nyingine ni Kenya, Afria Kusini, Morocco, Misri, Zambia, Gabon, Mauritius, Sierra Leone, Namibia na Zimbabwe.
Pia kuna nchi za Tunisia, Senegal, Ivory Coast, Botswana, Malawi na wenyeji Uganda. Mashindano hayo yatafanyika kwenye uwanja wa Lake Victoria Serena Golf Resort na Spa.