Gidabuday kuzikwa Jumamosi Katesh

Muktasari:
- Gidabuday aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), amefariki alfajiri ya kuamkia jana Septemba 10, 2024 baada ya kugongwa na gari jijini Arusha.
MWILI wa Wilhelim Gidabuday utapumzishwa kwenye nyumba yake ya milele Jumamosi kijijini kwao Nangwa, Katesh.
Gidabuday aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), amefariki alfajiri ya kuamkia jana Septemba 10, 2024 baada ya kugongwa na gari jijini Arusha.
Mdogo wa marehemu, Julius Gidabuday alisema safari ya kwenda Katesh mkoani Manyara itaanza Ijumaa jioni na Jumamosi kaka yake atazikwa.
Akizungumzia tukio la ajali, alisema hadi sasa hajafahamika mtu wala gari lililomgonga.
"Ilikuwa ni usiku saa 7 (usiku) alipokuwa akivuka barabara eneo la Maji ya Chai kwenda nyumbani kwake ndipo aligongwa na gari na aliyemgonga tunaelezwa alikimbia," alisema Julius.
"Kaka yetu alifia palepale, tulipigiwa simu na wasamaria wema kupitia simu yake."
Alisema mwili wa Gidabuday upo mochwari na msiba upo nyumbani kwake katika eneo la Maji ya Chai.
Hadi mauti yanamkuta, Gidabuday alikuwa katibu wa Kamati ya Mabadiliko ya Katiba ya RT, ambayo ilikuwa inaelekea ukingoni kukamilika.
Pia aliwahi kuwa mwanaharakati wa michezo kabla ya kuwa katibu mkuu wa RT wakati wa uongozi wa Anthony Mtaka hadi 2021.