Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fumbo la dakika 450 linalotishia historia ya Yanga

YANGA Pict


NDANI ya misimu minne iliyopita ambayo Yanga imetawala soka la Tanzania kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mfululizo, jambo moja limeendelea kujitokeza kila mwaka ambapo ni uwezo wao wa kufunga mabao.


Takwimu zinaonyesha namna kikosi hicho cha Wananchi kilivyobadilika kutoka timu inayoshinda kwa matokeo madogo hadi kuwa mashine ya kutengeneza mabao, hali inayoweka katika mtego wao wenyewe.


Msimu uliopita, Yanga ilitwaa ubingwa wake wa 31 wa Ligi Kuu Bara kwa kishindo baada ya kumaliza msimu ikiwa imefunga mabao 83. Idadi hiyo ilikuwa ongezeko la mabao 12 ukilinganisha na msimu wa 2023/24 ambapo walifunga mabao 71. Rekodi hiyo ndiyo inayosimama kama kiwango cha juu zaidi cha ufungaji kwa Yanga katika miaka ya hivi karibuni.

Safari ya mafanikio hayo ilianza msimu wa 2021/22, walipoivua Simba ubingwa waliokuwa wameutwaa kwa misimu minne mfululizo. Chini ya kocha Nasreddine Nabi, Yanga ilimaliza msimu huo ikiwa na pointi 74 huku ikifunga mabao 49 pekee na kuruhusu manane yakiwa ni machache zaidi kwenye misimu hiyo.

Ingawa mabao hayo hayakuwa mengi sana ikilinganishwa na misimu iliyofuata, yalitosha kuonyesha msingi wa timu iliyokuwa ikijengwa kwa nidhamu ya kiufundi na uimara wa safu ya ulinzi.

Katika msimu huo ambao Yanga katika kikosi chake ilikuwa na Fiston Mayele, Simba ilimaliza nafasi ya pili ilikusanya pointi 61 huku ikifunga mabao 41 na kuruhusu 14. Azam nayo ilimaliza nafasi ya tatu ikiwa na pointi 49, ikifunga mabao 41 na kuruhusu 28.

Msimu uliofuata wa 2022/23, Wananchi waliinua kiwango chao zaidi. Walitetea ubingwa kwa kukusanya pointi 78 huku wakifunga mabao 61 na kuruhusu 18. Hapa ndipo ilipoonekana wazi kuwa timu hiyo ilikuwa ikibadilika na kuwa na makali zaidi mbele ya lango. Ingawa Simba iliyokuwa nafasi ya pili ilifunga mabao mengi zaidi, 73, Yanga walibaki kuwa timu bora kutokana na matokeo yao ya jumla.

Azam kwa upande wake ilimaliza nafasi ya tatu ikiwa na pointi 59 huku ikifunga mabao 55. Hata hivyo, macho yote yalikuwa kwa Yanga ambao walikuwa wameongeza mabao 12 kutoka yale 49 ya msimu uliopita hadi kufikia 61.

Msimu wa 2023/24, maendeleo hayo yaliendelea kuonekana. Kutoka mabao 61 ya msimu wa 2022/23, Yanga ilipandisha kiwango na kufunga mabao 71. Hiyo ilikuwa ishara kuwa mfumo wao wa ushambuliaji ulikuwa unazidi kukomaa huku wachezaji wa safu ya mbele akiwemo Stephane Aziz Ki aliyekuwa mfungaji bora akiwa na mabao 21, wakiongeza mchango mkubwa katika kutafuta ushindi.

Makali hayo yaliongezeka zaidi msimu uliopita walipofikia mabao 83 na kuweka rekodi yao mpya ya ufungaji. Kila msimu umekuwa na ongezeko la mabao, jambo linaloonyesha kuwa Yanga imeendelea kuboresha ubora wa kikosi chake pamoja na mbinu za ushambuliaji.

Sasa, wakati msimu huu ukielekea ukingoni, Wananchi wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kuvunja rekodi hiyo. Hadi sasa, Yanga imefunga mabao 58 katika ligi, maana yake wanahitaji mabao 25 zaidi katika mechi tano zilizobaki ili kufikia idadi ya mabao 83 ya msimu uliopita na kuandika rekodi mpya.

Kihesabu, kazi hiyo si rahisi. Yanga italazimika kufunga wastani wa mabao matano kwa kila mechi iliyosalia. Hata hivyo, kutokana na ubora wa kikosi walichonacho na aina ya wapinzani waliobaki, bado kuna matumaini ya kuona wakikaribia au hata kuvunja rekodi hiyo ikiwa watakuwa na kiwango kizuri cha ufungaji katika mechi zao za mwisho.

Moja ya silaha kubwa waliyonayo kwa sasa ni kiungo mshambuliaji Allan Okello ambaye ameonyesha ubora mkubwa tangu ajiunge na timu hiyo katikati ya msimu. Okello tayari amefunga mabao 11 na kutoa asisti saba, akithibitisha kuwa ni mmoja wa wachezaji walioongeza ubunifu na hatari katika safu ya ushambuliaji ya Yanga.

Katika mechi tano zilizosalia, Juni 13, Yanga watakuwa wageni wa Mashujaa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika. Baada ya hapo, Juni 17 watasafiri tena kucheza dhidi ya Fountain Gate katika mchezo mwingine muhimu wa ligi.

Baada ya mechi hizo mbili, Yanga itahamishia nguvu zake kwenye Kombe la CRDB ambapo Juni 21 itakutana na Azam FC katika mchezo wa nusu fainali utakaopigwa jijini Mwanza. Kisha timu hizo zitakutana tena kwenye Ligi Kuu Bara siku tatu baadaye katika mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.

Mechi ya mwisho nyumbani kwa Yanga itakuwa dhidi ya TRA United Juni 27 kabla ya kucheza dhidi ya JKT Tanzania katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.

Mechi hizi ndizo zitakazoamua kama Wananchi wataendelea kuwa mabingwa wa rekodi au wataongeza historia nyingine.