Familia yakanusha kifo cha Kakake Hans Poppe

Tuesday September 14 2021
hanspope pic

KLABU ya Simba imeahirisha tukio la uzinduzi wa Wiki ya Simba kuelekea kilele cha Siku ya Simba, ‘Simba Day’ lililokuwa lianze jana kwa shughuli mbalimbali hadi itakapomaliza shughuli za mazishi ya aliyekuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe aliyefariki juzi usiku.

Mwili wa Hans Poppe jana uliagwa kwenye Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam kisha ulipelekwa Lugalo Hospitali ambako ulihifadhiwa kabla ya leo asubuhi kupelekwa nyumbani kwake Ununio kwa ajili ya familia kuaga na baadae mchana kusafirishwa kwenda Iringa tayari kwa mazishi.

Hata hivyo, familia imekanusha taarifa za kifo cha kaka mkubwa wa Hans Poppe iliyomtaja kwa jina la Eddy, ambaye juzi na jana ilivumishwa kwamba naye amefariki, ikiwa ni saa chache baada ya taarifa za kifo cha mdogo wake.

“Tulitaka kuweka sawa hili jambo, Eddy yupo hai, hajafariki kama inavyovumishwa ila hali yake si nzuri, amelazwa tumuombee aimarike na kuwa sawa,” alisema Mashaka Ndonde, mmoja wa wasemaji wa familia kwenye msiba huo.


SIMBA DAY

Advertisement

Kutokana na msiba huo mzito ambao umewatia simanzi wanasimba na wadau wa michezo kwa ujumla kutokana na Hans Poppe aliyojitolea enzi za uhai wake, klabu ya Simba imeeleza kusitisha shughuli zote za uzinduzi wa Simba Day iliyokuwa ianze jana kwa matukio mbalimbali kabla ya kilele Jumapili hii.

“Tumeahirisha shughuli zote hadi mazishi ya Hans Poppe yatakapomalizika,” alisema Crescentius Magori jana na kuongeza;

“Leo (jana) tumesoma dua kwa ajili ya Hans Poppe na wapendwa wetu wengine ambayo ilifanyika kwenye Uwanja wetu wa Bunju na kesho (leo), tutaungana na familia katika tukio la ibada ya mazishi.

“Japo tulitangaza ratiba ya Simba Day mapema, lakini haiwezi kuendelea hadi tukio la mazishi ya Hans Poppe litakapomalizika, bila shaka ratiba yetu itaendelea kati ya Jumanne au Jumatano,” alisema Magori.

Mwili wa Hans Poppe ambaye enzi za uhai wake alikuwa ni kiongozi wa Simba na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa klabu hiyo utazikwa Jumatano huko Kiheza Mkimbizi, mkoani Iringa.

Wadau mbalimbali wanaendelea kumlilia kutokana na mchango wake aliokuwa akiutoa enzi za uhai wake ikiwamo kwenye michezo na burudani, huku pia akiwa mmoja ya wafanyabiashara wakubwa nchini.

Advertisement