Edna Lema : Kocha Twiga Stars asimulia midume WAnavyosumbua

Muktasari:
- Edna anakubaliana na mabadiliko hayo na kusema awali ilikuwa ngumu kwao kuingia katika mchezo huo lakini sasa ni burudani.
MITAZAMO ya Kiafrika kwa muda mrefu ilikuwa soka ni mchezo wa wanaume tu. Bila shaka hilo limechangia kuchelewa kwa mafanikio ya timu zetu za wanawake Afrika ukilinganisha na timu za mataifa ya Ulaya na Amerika, ambako tayari mpira unapigwa mwingi sana.
Wakati mitazamo hiyo ikiwa imeanza kupungua Afrika, tayari Tanzania nako mambo yameanza kuwa ni ‘hivi’... mambo ni moto!
Tanzania sasa ni miongoni mwa nchi zinazokuja juu kwa kufanya vizuri kwenye soka la wanawake kwa kuwa na wachezaji wa kiwango kikubwa wanawake, makocha wanawake wanaofanya vizuri sambamba na kuchezwa kwa ligi za ngazi tofauti.
Edna Lema ni miongoni mwa makocha wanawake wanaofanya vizuri na yuko kwenye benchi la ufundi la timu ya taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’ akiwa msaidizi Kocha mkuu, Bakari Shime ‘Shetani Mweusi’.
Edna anakubaliana na mabadiliko hayo na kusema awali ilikuwa ngumu kwao kuingia katika mchezo huo lakini sasa ni burudani.
SOKA LA WANAWAKE UHUNI
Edna anaelezea kwa undani mtazamo ambao hata yeye wakati anaingia kwenye soka aliukuta.
“Jambo zuri kwa Watanzania ni kupungua kwa dhana iliyozoelekea awali kuwa mpira wa miguu kwa wanawake ni uhuni. Nina imani sasa hivi kwa Tanzania asilimia 60 ya watu wanauelewa, wanacheza na wanakuja uwanjani kwa wingi,” anasema Edna.
Anasema, kitu kikubwa ambacho kimewafanya Watanzania kuulewa mpira huo kwa wanawake ni ligi inayoendeshwa nchini lakini akapendekeza wadau wengi kujitokeza kwa wingi hasa wadhamini.
“Jambo la kufurahisha, wadau sasa wameanza kutambua umuhimu wa soka la wanawake kuwa ni ajira pia ni fani au burudani kwa watu wote kama zilivyo nyingine za muziki au kuogelea,” anasema Edna.
“Kama ambavyo unaona sasa, hata ukienda uwanjani asilimia kubwa ya wanawake wanakwenda kuangalia mpira wakiwa huru na kila mtu anachukulia kawaida tu.”
KUCHEZA NA WANAUME
Edna ambaye ni mama wa mtoto mmoja wa kiume aitwaye Eann (9) anasema, alianza kupenda mpira tangu alipokuwa binti mdogo kwao Moshi.
“Kaka zangu ndiyo walikuwa wananichukua na kwenda nao mazoezi na huko ndiko nilipoanza kujifunza kucheza mpira taratibu hadi nikawa mtaalamu,” anasema Edna ambaye anacheza kwa kutumia miguu yote miwili.
Ameongeza kuwa hata alipohama kutoka Moshi na kwenda Morogoro alikuwa anacheza na wanaume pia.
WANAUME WAMMEZEA MATE
Edna, mwanadada mwenye mvuto, anasema katika kazi yake hiyo ya soka anakutana na changamoto nyingi ndani na nje ya kikosi .
“Asilimia kubwa ya watu wanakuwa hawakuelewi. Wanajiuliza kwa nini unacheza mpira wa miguu, lakini wanakuja kupata majibu wakati ambao matunda yanaanza kuonekana,” anasema Edna.
“Changamoto nyingine ni hii. Unapoanza kujulikana na umaarufu kidogo si unajua tena sisi wanawake, wanaume wanaanza kukufata kwa ajili ya uhusiano jambo ambalo kama hauko makini ni ngumu kufikia malengo.”
Anasema changamoto nyingine hali ya kujuana ambayo baadhi ya wachezaji hutaka kuipa nafasi.
Edna anasema ameingia kufundisha timu ambayo ina wachezaji ambao awali alicheza nao hivyo baadhi wanamchukulia poa kama kumtania na mambo mengine na hata wanapopanga timu, si wote ambao wanakubalina na kikosi hicho.
“Utakuta watu wanakwambia kwa nini yule hajapangwa au hachezi na huyu kwa nini anaanza. Hiyo inakuwa ni kwa ajili ya maono na mapenzi yake lakini kwa sababu katika mafunzo ya kazi yetu tunafundishwa mambo mengi, na yote hayo unachukulia kama sehemu ya changamoto,” anasema.
“Katika hilo huwezi kuwafuata mashabiki au watu hao wanataka nini kwa sababu maisha ya kazi ni sawa na ndoa, hawajui ndani ya kambi na katika maandalizi yetu tunaishi vipi na tunafanyaje kazi.”
KUTOTUMIA KILEVI
Edna anasema amecheza soka kwa kipindi kirefu na kutembea sehemu mbalimbali lakini hajaweza kutumia kilevi cha aina yoyote.
“Kwangu naweza kusema ni bahati nzuri kutokana na mazingira ya mpira kama unavyojua katika maisha hayo mara nyingi yanakuwa na changamoto nyingi. Namshukuru Mungu sikutumia kilevi cha aina yoyote, si muumini wa kupenda kwenda kwenye kumbi za starehe kucheza muziki kwa wingi na si muhuni,” anasema Edna.
“Furaha yangu ni kuangalia soka kwenye televisheni, uwanjani na wakati mwingine kucheza si unajua unakumbushia enzi kwa ajili ya mazoezi binafsi pamoja na kusikiliza muziki.”
AKUTANA NA MACHUPA
Edna anasema: “Nakumbuka ilikuwa kama mwaka 2000, Mzee Machupa (sasa ni marehemu) alikuja Morogoro kwa ajili ya kutafuta wachezaji wa timu ya taifa hapo ndipo aliniona na kunichagua, ukawa mwanzo wa safari ya Dar es Salaam.”
Anasema alipochukuliwa Twiga Stars alikuwa binti mdogo hivyo akawa anakaa wenzake kwa ajili ya kupata uzoefu na si kucheza. Kucheza kulikuja baadaye.
Kocha huyo mbali na kulelewa na kituo cha Moro Kids anazitaja klabu alizozichezea ni pamoja na Polisi Morogoro wanawake, Vijana Mburahati na Mchangani Sisters ya Mwananyamala.
KILICHOMSTAAFISHA SOKA
Anasema, baada ya kucheza soka kwa kipindi kirefu aliamua kustaafu rasmi kucheza timu ya taifa ‘Twiga Stars’ mwaka 2007.
Anasema alicheza soka kwa kipindi cha takribani miaka sita lakini alikutana na mambo yaliyomfanya atundike daluga.
“Sababu kubwa ya mimi kustaafu ni maumivu ya mguu. Niliumia goti nikakaa nje ya uwanja kwa muda mrefu hata niliporudi uwanjani hali haikuwa nzuri. Pia vijana wadogo walikuwa wanachipukia kwa wingi hivyo nikaona ni bora nikae pembeni kupisha watu wengine,” anasema Edna.
“Unajua wakati mwingine ukiona mambo hayaendi vizuri ni bora ufanye maamuzi magumu na si kusubiri hadi watu wakuzomee.”
AJIKITA KWENYE KILIMO
Anasema, baada ya kustaafu aliamua kusoma kozi tofauti za ukocha, akafanya biashara pamoja na kilimo.
“Mimi ni mkulima kule Morogoro, nalima mahindi, vitunguu pia nafuga kuku wa nyama wa biashara wa Kizungu. Huwa nanunua wadogo nawakuza kisha nawauza,” anasema Edna, ambaye ameweka wazi katika biashara yake ya kuku alifanikiwa kufuga hadi kuku 500 kwa mkupuo na kuwauza. Anasema, kazi hizo zimemsaidia kuongeza kipato chake.
ARUDI STARS AKIWA KOCHA
Akizungumzia namna alivyojiendeleza katika hadi kuwa kocha, anasema alipata kozi mbalimbali. “Nilianza na kozi ya awali, ya kati na kusomea leseni C. Nilijiendeleza kwa kusoma kozi hizo na baada ya kumaliza leseni C, mwaka 2015 niliitwa kuifundisha Twiga Stars kwa ajili ya kupata uzoefu zaidi. Niliambiwa kwa sababu nilicheza kwa kiwango cha juu na nina uwezo katika kufundisha ni vyema nikawa na timu hiyo kwa ajili ya kupata uzoefu zaidi na ndiyo ukawa mwanzo.”
Edna ambaye sasa ana leseni B, pia ni kiongozi wa Chama cha Soka Mkoa wa Morogoro kwa wanawake anafafanua:
“Wanawake wa Morogoro wameniona nafaa hivyo walichagua nikawa mwenyekiti wao nafasi ambayo nimeishika kwa kipindi kirefu na naendelea kuishikilia.”
Kazi ya ukocha hakusomea tu nchini, alivuka hadi bahari kwenda kupokea maujuzi kwengineko. Unataka kujua ni kocha gani anamkubali, pia ndani ya uwanja kuna nyota akiwaangalia wanamkosha kweli.
Unajua pia amesomea ukocha nje ya nchi na sio hapa Afrika, bali Ulaya. Ungana naye kesho Ijumaa kujua mengi zaidi.