Dili la Badru lakwama Songea United

Muktasari:

  • Badru ambaye aliwahi kuzifundisha Gwambina United na Mtibwa Sugar kwa nyakati tofauti wakati zikiwa Ligi Kuu Bara, alisema kulikuwa na zaidi ya asilimia 70 za yeye kujiunga na timu hiyo ambayo zamani ilikuwa ikifahamika kama FGA Talents kabla ya mambo kuwa tofauti.

ALIYEKUWA kocha wa timu za vijana za Azam FC, Mohammed Badru amesema dili lake kutua Songea United limeota mbawa na badala yake imembidi kutoa sapoti kwa viongozi wa chama hilo kutokana na heshima yao kwake, hivyo ilimbidi kuandaa programu mbalimbali za mazoezi kama sehemu ya maandalizi yao kwa ajili ya msimu ujao wa Championship.

Badru ambaye aliwahi kuzifundisha Gwambina United na Mtibwa Sugar kwa nyakati tofauti wakati zikiwa Ligi Kuu Bara, alisema kulikuwa na zaidi ya asilimia 70 za yeye kujiunga na timu hiyo ambayo zamani ilikuwa ikifahamika kama FGA Talents kabla ya mambo kuwa tofauti.

“Ni kweli kwamba nilikuwa na timu lakini ilikuwa ni kwa ajili ya kuisapoti tu,nilikuwa na programu nao za mazoezi ya nguvu ili kupunguza mafuta wachezaji maana wametoka likizo ili kuwa na nguvu ya kuanza msimu ujao wa Championship,” alisema kocha huyo na kuongeza:

“Tulikuwa na mazungumzo ya kusaini mkataba lakini mambo hayakwenda vizuri (ya kimkataba) na kwa sababu mimi ni mtu wa mpira niliona kuwa sio mbaya wakati wakiendelea na mpango wa kutafuta kocha nifanye programu ambayo itakuwa kama msingi ambao utaendelezwa tu.”

Kocha huyo aliongeza kwa tathimini ambayo aliifanya kwenye kikosi hicho, Songea United wanaweza kupanda ligi kuu kutokana na aina ya wachezaji walionao, kikubwa ni viongozi kutoa sapoti ya hali na mali.

Msimu uliopita wa Championship, Songea United ambayo zamani ilikuwa FGA Talents ilishika nafasi ya 10 kwenye msimamo wenye timu 16 huku ikijikusanyia pointi 34 katika michezo 30. Walizidiwa pointi 33 na Pamba ambayo ilipanda ligi kuu kama washindi wa pili.