Dewji aitakia kheri Yanga

Muktasari:

  • Dewji amesema yeye aliwahi kuwa sehemu ya mafanikio ya Simba ilipocheza fainali 1993 akiwa kama kiongozi ndani ya timu hiyo lakini hawakuchukua ubingwa.

ALIYEKUWA mfadhili wa Simba, Azim Dewji ameitakia kheri klabu ya Yanga inafanya vizuri kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kisha kuchukua ubingwa ili kuweza kuitangaza nchi ya Tanzania.

Dewji amesema yeye aliwahi kuwa sehemu ya mafanikio ya Simba ilipocheza fainali 1993 akiwa kama kiongozi ndani ya timu hiyo lakini hawakuchukua ubingwa.

"Hii sio rekodi ya kwanza kuwekwa hapa Tanzania kwa sababu mimi nilishawaji kuiweka nikiwa na Simba miaka 30 nyuma, ile ni historia na ishapita ila kwa sasa tunaangalia hapa kwa Yanga;

"Nawatakia kheri waweze kuchukua ubingwa kwa sababu itakuwa rekodi nzuri kwao na kwa Hersi (Said) kama ilivyokuwa kwangu mimi na Simba katika miaka hiyo ya nyuma."

Dewji amesema Simba sio timu mbaya lakini waliteleza kwenye robo fainali lakini mashabiki wengi wanaona kama timu hiyo sio nzuri jambo ambalo sio la kweli.

"Simba na Yanga ni timu kubwa zote hapa Afrika, ila mashabiki huwa wanalinganisha timu hizi pindi mmoja anapofanya vizuri jambo ambalo wanakuwa wanakosea."

Simba ndio timu ya kwanza kucheza fainali za kombe la Shirikisho Afrika wakati huo likiitwa kombe la Caf na Simba ilifungwa na Stella Adjame 2-0.