Dereva wa Kalaba alikuwa mke wa rafiki yake

Muktasari:

  • Vyanzo mbalimbali vya habari Zambia vimeripoti Mkandawire ndiye aliyekutwa kwenye kiti cha dereva baada ya gari ndogo aina ya Mercedes Benz aliyokuwa anaendesha kugongana na Lori la mafuta, jana Kafue, jijini Lusaka, Zambia.

SIKU moja baada ya ajali mbaya ya gari aliyoipata mchezaji wa zamani wa TP Mazembe na timu ya taifa ya Zambia, Rainford Kalaba, inadaiwa mwanamke aliyekuwa naye wakati ajali hiyo inatokea, Charlene Mkandawire ni mke wa rafiki yake.

Vyanzo mbalimbali vya habari Zambia vimeripoti Mkandawire ndiye aliyekutwa kwenye kiti cha dereva baada ya gari ndogo aina ya Mercedes Benz aliyokuwa anaendesha kugongana na Lori la mafuta, jana Kafue, jijini Lusaka, Zambia.

Kwa mujibu wa ripoti Mkandawire alifariki dunia papo hapo huku Kalaba mwenye umri wa miaka 37, akiwahishwa hospitalini kupatiwa matibabu zaidi na hadi sasa hali yake bado ni mbaya.

Awali haikutambulika ni mwanamke gani aliyekuwamo kwenye gari hiyo hadi mapema hii leo zilipoibuka taarifa hizo kutoka Zambia.

Pia kumekuwa na video inayosambaa ikimwonyesha mwanamke huyo mrefu wa kimo akicheza muziki na kalaba.

Mkuu wa kitendo cha uhusiano wa nje wa University Teaching Hospital (UTH), huko Zambia amesema madaktari hospitalini hapo wanaendelea kufanya linalowezekana kuhakikisha mchezaji wa zamani wa TP Mazembe na timu ya taifa ya Zambia Rainford Kalaba anarudi katika hali yake.

Akizungumza akiwa Hosptalini hapo alisema Kalaba aliwasili kati ya saa tisa kuelekea saa 10 alasiri na alipokelewa na kuwahishwa wodi ya wagonjwa mahututi.

"Hali yake sio nzuri na madaktari wetu wanafanya kila liwezekanalo kuhakikisha anarudi katika hali yake, alipata ajali ya gari nafikiri kila mtu anafahamu hilo lakini tunapambana kadri tuwezavyo ili awe sawa na napenda kukanusha taarifa zinazotolewa na baadhi ya media kwamba amefariki, hapana ni mzima."

Kabla ya kustaafu soka Julai mwaka jana akiwa na Mazembe, Kalaba alikuwa mmoja kati ya mastaa tegemeo wa timu hiyo akiisaidia kuchukua taji la Ligi ya Mabingwa mwaka 2015.

Kalaba alikuwepo katika kikosi cha taifa hilo kilichochukua ubingwa wa AFCON mwaka 2012, ambayo yeye alicheza mechi saba kwa dakika 90 na hadi anastaafu kuichezea timu ya taifa mwaka 2018, alishacheza mechi 108 na kufunga mabao 14.

Kabla ya kutua Mazembe mwaka 2010, Kalaba aliwahi kupita timu mbalimbali barani Ulaya akianzia timu ya vijana ya Nice ya Ufaransa kisha Braga, Gil Vicente FC na Leiria zote za Ureno. Pale Zambia aliwahi kuzichezea Kitwe United na Zesco.