Dabi ya Kariakoo yawaibua wabunge, wataka uwazi

Muktasari:
- Kelele za kununuliwa kwa mechi na na wanasiasa kuingilia sheria za ligi zimewafanya wabunge waape kushika shilingi wakitaka majibu ya kuipa heshima ligi kuu
Wabunge wameishukia Wizara ya Habari,Sanaa, Utamaduni na Michezo wakitaka itoe majibu ya kina katika mambo matatu likiwemo la kuifanya Bodi ya Ligi (TPLB) ijitegemee badala ya kuwa chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Mengine ni kutaka uwazi wa nini kinachoendelea kuhusu mazungumzo ya viongozi wa Timu za Simba na Yanga pamoja na serikali kuhusu dabi na kwa nini imekuwa kimya.
Jambo lingine lililopigiwa kelele ni kilichotajwa kuwa siasa zimeingia kwenye mpira hata kusababisha kiwango cha mpira kushuka wakifananisha na Ligi ya Italia ambayo wanasema imepoteza mvuto.
Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma ameliamsha leo Jumatano Mei 7,2025 wakati akichangia kwenye Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Wizara ya Habari katika maombi ya fedha ya mwaka 2025/26.
Msukuma amemtaka Waziri wa Michezo, Profesa Paramagamba Kabudi kueleza alichokutana nacho ndani katika kikao cha maridhiano ya Simba na Yanga ambacho kilimfikisha saa nne za usiku.
Wizara imeomba Sh519.66 bilioni, huku wabunge wakitofautiana kuhusu utendaji wa TFF wengine wakipongeza na wengine kuponda kuwa wanayumbisha ligi.
Msukuma amewataka viongozi wa TFF kuiga mfano wa Rais wa zamani wa TFF, Leodgar Tenga aliyemuelekeza kama aliyefanya kazi nzuri inayopaswa kuigwa hata kumfanya aendelee kuheshimika katika tasnia ya michezo nchini.
“Alifanya kazi vizuri na ni mfano wa kuigwa, muige mfano jinsi alivyoongoza anaheshimika vinginevyo mtamaliza vipindi vyenu halafu mtakuwa mahohehahe hamjulikana mlichofanya,” amesema Msukuma.
Amemtaka Waziri wa Michezo, Profesa Kabudi kueleza kinagaubaga nini alichokutana nacho ndani ya kikao kilichowakutanisha viongozi wa Simba na Yanga ambacho kilimuweka hadi saa nne za usiku kwani imekuwa ni fumbo wakati watu wanataka kujua.
“Ulichokisikia tueleza nasi tusikie ili tukawajulishe wananchi wetu, mpira wa Simba na Yanga ndiyo furaha, lakini kunapokuwa na migogoro halafu mnakuwa kimya na sijaona mahali popote ulipotaja migogoro hiyo hata mahali pamoja wakati Rais anajua mambo ya michezo na ametoa ndege kuwapeleka Simba Morocco,” amesema.
Amekataa alichokisema ni kuendelea kusikiliza ngonjera ngonjera za huku na huku kule huku tena zinasikika habari za dabi akahoji hiyo dabi itachezwa na bodi ya ligi au Yanga.
Ametumia kauli ya “halafu unakutana na viongozi wahuni tu, hatuwezi kukubali, wote humu tunaweza kuwa marais wa TFF na hata mimi naweza kuteuliwa kuongoza.”
Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Hamisi Taletale 'Babu Tale' ametupa dongo kwa wanasiasa kuwa wanaharibu mpira wa Tanzania kwa kuingilia mambo, huku akiwakumbusha kuwa itafanana na Ligi ya Italia ambayo sasa imepoteza mvuto.
Babu amesema inashangaza Simba na Yanga huwa hazifungwi jambo alilosema sio sawa lakini akatolea mfano kwenye ligi ya Muungano namna Yanga ilivyopata ushindi kwa jasho.
“Viongozi simamieni sheria, bila kusimamia sheria tunakwenda kuua mpira, acheni kutengeneza utaratibu ambao tunaona hawa wanabebwa, wakicheza hapa utasikia Yanga kampiga mtu tano Simba kapiga saba lakini wakitoka nje ujue jini katoka mganga hoi,” amesema Babu Tale.
Akizungumzia dabi, amesema bila kufuata sheria itawayumbisha, kwani anakurupuka mtu mmoja aliyevaa tai na kusema ‘hatuchezi’ jambo alilosema sio sawa kabisa.
Katika hatua nyingine amelalamikia mfuko wa wasanii ambao ameeleza, Rais ameweka fedha kwa wasanii, lakini wizara imezirudisha benki ikafanya ziwe na masharti magumu ya kukopa hadi kwa dhamana ya nyumba ambazo zmeeleza hakuna wasanii wenye nyumba.
Kwa upande wake Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda amesema kuna matatizo makubwa ndani ya mfumo wa Ligi ya Tanzania ikiwemo kukosekana kwa uadilifu.
Mbunge huyo amesema watu wanajali Simba na Yanga badala ya kujali mpira wa miguu kwa ujumla wake na ndilo tatizo timu zingine zinacheza kwa alichosema kuna kitu nyuma ya pazia.
Kakunda ametaka sababu za kuahirishwa kwa dabi ziwekwe hadharani kwani mamlaka zilisema wanafanya uchunguzi hivyo ielezwe wazi ni uchunguzi upi uliofanywa na Watanzania wajue.
“Sheria 17 zinalegezwa, marefalii wanapewa adhabu za ajabu ajabu lakini sheria zikisimamiwa na kuwa bora itasaidia kuliko kuwa na sheria za makaratasi,” amesema Kakunda.