Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Clara Luvanga namba zimempa heshima Saudia

Muktasari:

  • Mambo ambayo ameyafanya msimu huu hasa kuwatesa mabeki na makipa wa timu pinzani kwa mabao ya mbali yamempa sifa kubwa nyota huyo wa Kitanzania.

KAMA kuna msimu bora kwa mshambuliaji wa Kitanzania, Clara Luvanga anayeitumikia Al Nassr ya Saudia basi ni huu.

Mambo ambayo ameyafanya msimu huu hasa kuwatesa mabeki na makipa wa timu pinzani kwa mabao ya mbali yamempa sifa kubwa nyota huyo wa Kitanzania.

Sio jambo la ajabu kumuona nyota huyo akionyesha kiwango bora kwani amekuwa akifanya hivyo kwa wanaomkumbuka kwenye mashindano ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa wanawake chini ya miaka 17 alitikisa nyavu hasa kiasi cha Cameroon kugoma kuingiza timu kwa moto aliouonyesha mwaka 2022.

Kati ya rekodi alizoweka nyota huyo akiwa na umri mdogo ni kufunga mabao 10 katika mashindano yale na kufunga hat-trick kwenye mechi dhidi ya Cameroon.

Hayo ni baadhi tu ya yale aliyoyafanya akiwa na jezi ya timu ya taifa ya U17 ya Serengeti Girls na ameendelea kuonyesha maajabu yake akiwa na kikosi cha Al Nassr.

Nguvu, kasi na uwezo wa kufunga mabao kwa mashuti makali ni kati ya sifa alizobarikiwa mwanadada huyo miguuni mwake.

Wikiendi iliyopita Al Nassr ilikabidhiwa ubingwa rasmi wa SWPL ukiwa wa tatu mfululizo kwa klabu hiyo lakini wa pili kwa Clara.

Kabla ya kuichezea Al Nassr aliwahi kuzitumikia klabu mbalimbali kama Dux Lugrono ya Hispania na Yanga Princess.

Haya ni baadhi ya makubwa aliyoyafanya Clara ndani ya misimu miwili aliyoitumikia Al Nassr.


MSIMU ULIOPITA

Alichokifanya kwenye msimu wake wa kwanza ulithibitisha ubora wa nyota huyo kwenye kufumania nyavu za makipa wa timu pinzani.

Kama mshambuliaji anayeanza kwenye kikosi hicho, msimu wa kwanza aliiwezesha Al Nassr (W) kutetea taji la ligi kwa kufunga mabao 11 na asisti saba kwenye mechi 12 alizocheza

Katika mabao hayo 11 aliyofunga alitupia hat-trick mbili dhidi ya Al Ula na Eastern Flames, na pia alishinda tuzo ya goli bora la mwezi Desemba 2023 dhidi ya Al Hilal.​


MABAO YAKE

Msimu huu ameendeleza pale alipoishia akimaliza na mabao 20 na asisti saba kwenye ligi nyuma ya kinara Ajara Nchout (Al-Qadsiah) na Ibtissam Jraidi (Al-Ahli) waliofunga mabao 24 kila mmoja.

Hakuna bao la penati alilofunga na mabao yote ni yale ya kideoni akiwapindua makipa kupiga kwa mashuti makali.

Kama kuna timu ambayo mshambuliaji huyo amekuwa akiionea kila anapokutana nayo basi ni Eastern Flames iliyomaliza nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi.

Tangu msimu uliopita Clara alifunga hat-trick kwenye mchezo na Flames na msimu huu aliifunga mabao manne kwenye ushindi wa 7-0 Januari 31.

Flames ni chama la zamani la Mtanzania mwenzake, Enekia Lunyamila aliyeichezea msimu uliopita na sasa anakipiga Mazaltan FC ya Mexico.

Timu nyingine ambayo Clara aliifunga hat-trick msimu huu ni Al-Taraji iliyomaliza mkiani, kwenye ushindi wa mabao 6–0, April 23.

Hata hivyo, msimu huu aliibuka na tuzo moja ya Bao Bora la Wiki kati ya mabao matatu ya hat-trick dhidi ya Al Taraji.

UBINGWA WA PILI

Makubwa mengine ni nyota huyo kubeba ubingwa wa pili mfululizo akiwa anasakata kabumbu ugenini kwani kwenye maisha yake ya soka hajawahi kubeba ndoo.

Mabao yake yameifanya Al Nassr kucheza mechi 16 bila kupoteza mchezo wowote ukiwa ubingwa wa pili kwa Clara na wa tatu mfululizo kwa kwa klabu hiyo.


PACHA WA LINA

Timu hiyo imesajili wachezaji mbalimbali wa kimataifa akiwemo kiungo mshambuliaji Lina Boussaha aliyekipiga PSG, Lille na timu ya taifa ya Ufaransa.

Eneo la ushambuliaji ukimtoa Luvanga kuna Mubarkh Al-Saiari raia wa Saudia, Mbrazili Duda Francelino na Mkongomani Ruth Kipoyi.

Lakini nje ya ubora wa nyota hao Luvanga alitengeneza pacha bora na Lina miongoni mwa wachezaji ghali nchini Saudia.

Katika mabao 11 aliyofunga Lina msimu huu Clara ametoa asisti tano kiufupi ni miongoni mwa pacha za ushambuliaji zinazoelewana.

Na pia, katika mabao 20 ya Clara nyota huyo raia wa Algeria ametoa asisti tano.

MSIKIE MWENYEWE

Akizungumza na Mwanaspoti baada ya kunyanyua ndoo hiyo ya pili mfululizo, Clara anasema: “Ninafurahi kuwa mmoja wa wachezaji walioipa timu ya Al Nassr ubingwa pia kwangu mimi hii nzuri sana, asante Mungu.”