Chipukizi hali tete, shabiki afungiwa
TIMU ya soka ya Chipukizi imeendelea kuwa na wakati mgumu kwenye Ligi Kuu Zanzibar, baada ya kuendelea kufanya vibaya kwenye mashindano hayo.
Chipukizi ilikubali kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Jamhuri, kisha ikatoka sare ya bila kufungana na maafande wa Hard Rock na kufungwa bao 1-0 na maafande wa Kipanga katika michezo iliyopigwa Uwanja FFU Finya.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha wa timu hiyo Mzee Ali Abdalla alisema: “Unajua sisi tumefungwa, lakini moja ya sababu inayotufanya tufungwe ni kutokana na baadhi ya wachezaji wetu ni wageni wa ligi hiyo.”
Mzee alieleza kuwa bado wana mikakati ya kumaliza ligi katika nafasi mbili bora za juu ili kurejesha heshima ya timu hiyo.
Nahodha wa timu hiyo, Abdul-Mahafudh aliwataka mashabiki na wapenzi kuendelea kuwasapoti ili wafanye vizuri katika michezo inayofuata.
Katika hatua nyingine, Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka Zanzibar (ZBL) imeitoza faini ya Sh200,000 timu ya Mwenge ya Wete baada shabiki wake, Seif Abdalla Said kudaiwa kufanya kitendo cha utovu wa nidhamu.
Shabiki huyo alifanya kitendo hicho katika mechi ya Ligi Daraja la Kwanza Kanda ya Pemba dhidi ya Kizimbani iliyochezwa kwenye Uwanja wa FFU Finya.
Shabiki huo anadaiwa kufanya vurugu pamoja na kutishia kumpiga kwa mpira mwamuzi wa mchezo huo jambo ambalo limeelezwa sio la kimichezo. Pia amefungiwa kuingia uwanjani kushuhudia mechi za soka zote.
Shabiki huyo amepewa adhabu kwa mujibu wa sura ya 19 ya kifungu cha kwanza (1) na cha pili (2) na cha (3) mabano (ii) cha kanuni zinazoongoza soka msimu huu.