Chama apokelewa kimafia Bongo

WAKATI Mashabiki wengi wa Simba wakiwa nje ya Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Dar es Salaam kumsubiri nyota wao mpya Mzambia, Clatous Chama awasili, viongozi wa timu hiyo wamempokea kimafia.

Jioni ya leo kupitia ukurasa rasmi wa Mtandao wa kijamii wa Instagram, Simba iliweka video ikimuonesha Chama kuwa Uwanja wa Ndege wa Zambia tayari kwa safari ya kuja Bongo na kuweka bayana kuwa atawasili saa 12, za jioni.

Muda huo ulivyofika, kweli Chama aliwasili sambamba na wasafiri wengine lakini viongozi wa Simba waliokuja kumpokea wakiongozwa na mratibu wa timu hiyo, Abbas Ally walimpokea kimafia na kufanya asionwe na mashabiki wala waandishi wa habari waliokuwa nje ya Uwanja huo.

Chama baada ya ku-scan mizigo, alitolewa kupitia mlango wa VIP ambao mara nyingi hupita viongozi wakubwa wa Serikali na watu mashuri jambo ambalo limewafanya mashabiki wa Simba waliokuwa nje ya Uwanja huo kubaki wameduwaa.

Wakati Chama akitolewa kimya kimya ndani ya Uwanja huo, moja ya viongozi wa Simba sekta ya habari ‘Chico’ alikuwa akizunguka kwenye mlango wa kutokea jambo lililowafanya mashabiki wale kuamini kuwa Mwamba wa Lusaka bado yupo ndani.

Mashabiki wale walikata tamaa ya kumsubiri Chama baada ya kuona picha zake zikiwa zimechapishwa kwenye kurasa ya Instagram ya Simba ndio wakaondoka kila mmoja na pozi lake.

Chama amerejea Simba baada ya kuondoka mwishoni mwa msimu uliopita na kujiunga na RS Berkane ya Morocco ambako hakuwa na furaha na kukubaliana kuachana kwa amani.