Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chama aibeba tena Simba ikirejea kileleni

Muktasari:

  • Asisti mbili za kiungo huyo wa Zambia kwa mabao ya Libasse Gueye dakika ya 36 na la Alain Anicet Oura dakika ya 44, yametosha kuipa timu hiyo ushindi wa 2-1, dhidi ya Coastal Union, katika mechi ya Ligi Kuu iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini, Tanga na kumfanya Chama aibuke tena mchezaji bora wa mchezo kwa mara ya tano mfululizo.

UNAPOTAJA miongoni mwa wachezaji hatari wa Simba kwa sasa, hutoacha kulitaja jina la nyota wa kikosi hicho, Clatous Chota Chama 'Triple C', baada ya kuirejesha tena timu hiyo kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, baada ya kusota kwa muda mrefu.

Asisti mbili za kiungo huyo wa Zambia kwa mabao ya Libasse Gueye dakika ya 36 na la Alain Anicet Oura dakika ya 44, yametosha kuipa timu hiyo ushindi wa 2-1, dhidi ya Coastal Union, katika mechi ya Ligi Kuu iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini, Tanga na kumfanya Chama aibuke tena mchezaji bora wa mchezo kwa mara ya tano mfululizo.

Coastal Union ilianza kuishtukiza Simba kwa bao la dakika ya nane tu lililofungwa na mshambuliaji nyota wa kikosi hicho, Maabad Maulid aliyekutana na mpira ukizagaa katika lango la timu hiyo ya Msimbazi na kupiga shuti kali la moja kwa moja.

Hata hivyo, Simba ilijibu majibu hayo kwa kutengeneza mashambuliaji katika lango la Coastal Union, ambapo ilipata bao la kwanza kupitia Libasse Gueye, kisha, Anicet Oura akaandika la pili kwa kichwa akimaliza mpira wa kona ya Clatous Chama.

Mabao hayo mawili ya Simba yametokana na ustadi mzuri wa Chama ambaye tangu amerejea ndani ya kikosi hicho Januari 2026, akitokea Singida Black Stars, tayari amehusika katika mabao 12 ya Ligi Kuu Bara.

Chama aliyerejea msimu huu kwa mara ya tatu katika kikosi hicho, kiujumla amehusika katika mabao 14, akifunga sita akiwa na Simba na mawili akiifungia Singida Black Stars, huku akitoa asisti sita zote akicheza timu hiyo ya mitaa ya Msimbazi.

Kwa upande wa Libasse Gueye aliyejiunga na timu hiyo dirisha dogo la Januari 2026 akitokea Teungueth FC ya kwao Senegal, amefikisha bao lake la sita la Ligi Kuu Bara akiwa na kikosi hicho, ikiwa ni mwendelezo mzuri tangu asajiliwe kikosini.

Kwa Anicet Oura raia wa Ivory Coast aliyejiunga pia na timu hiyo dirisha dogo la Januari 2026, akitokea IF Gnistan ya Finland, ameendeleza kiwango kizuri tangu ajiunge na kikosi hicho, baada ya kufikisha bao lake la nne msimu huu la Ligi.

Bao la mshambuliaji wa Coastal Union, Maabad Maulid limemfanya pia nyota huyo kufikisha mabao sita ya Ligi Kuu msimu huu akiwa ndiye kinara wa kikosi hicho cha 'Wagosi wa Kaya' akiivunja rekodi yake ya msimu uliopita aliofunga mabao matano.

Ushindi huu kwa Simba unaifanya timu hiyo kuongoza katika msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha pointi 55, baada ya kucheza mechi 24, ambapo kati ya hizo imeshinda 16, ikitoka sare saba na kupoteza moja, huku ikifunga mabao 44 na kuruhusu 10.

Simba imerejea kileleni kwa mara ya kwanza tangu mara ya mwisho Novemba 9, 2025, iliposhushwa na Yanga ambapo kwa sasa vita yao ya kubadilishana pale juu imeanza kupamba moto zikibaki mechi sita kwa saba kumaliza msimu huu.

Yanga iliyokaa kileleni kwa muda mrefu ikipishana na maafande wa JKT Tanzania na Mbeya City kabla ya timu hizo kuishiwa nguvu mwishoni, kwa sasa iko nafasi ya pili na pointi 54, ikishinda mechi 16, sare sita na kupoteza moja tu kati ya 23.

Kwa upande wa Coastal Union, inaendelea kubakia nafasi ya 12 na pointi 25, ikishinda mechi sita, sare saba na kupoteza 11, ikiendeleza rekodi mbovu dhidi ya Simba katika Ligi Kuu, tangu mara ya mwisho iliposhinda bao 1-0, Machi 23, 2014.

Mechi ya kwanza kwa timu hizo kukutana ilikuwa ni Aprili 2, 2026, ambapo Simba ilishindi kwa mabao 2-0, yaliyofungwa na nyota wa kikosi hicho, Seleman Mwalimu 'Gomez' dakika ya 25 na beki wa kati, Ismael Olivier Toure aliyefunga dakika ya 45+2.