Casillas aipinga tuzo ya Lionel Messi, amtaja Iniesta
Muktasari:
Messi alinyakua pointi 853 ambayo ilikuwa ni asilimia 22.65 ya kura zote akifuatiwa na Andres Iniesta asilimia 17.36 na Xavi Hernandez asilimia 16.48.
Katika toleo lililopita mwandishi Luca Caioli alizungumzia tukio la Messi kutwaa tuzo ya kwanza ya Ballon d’Or lilivyokuwa na kugusia kidogo madai kwamba tuzo hiyo ilitakiwa kwenda kwa staa mwenzake wa Barcelona, Andres Iniesta. Sasa endelea…
Siku chache baadaye Pep alipoulizwa kuhusu uvumi ulioenea kwamba Iniesta ndiye aliyetabiriwa kuwa mshindi, Pep alijibu kwa kifupi, “Nafikiri Messi ni mchezaji bora.”
Akiwa kama aliyechanganyikiwa, kijana mdogo kutoka Rosario aliinuka haraka na kufunga vifungo vya koti lake la suti ya Dolce & Gabbana, akaweka vizuri tai yake shingoni na kutoa kidogo ulimi wake nje kama anavyofanya Michael Jordan anaporuka juu kufunga katika mpira wa kikapu na kupanda jukwaani.
Habari za jioni wote na asanteni kwa kunipongeza,” alisema Messi na kuongeza, “Ukweli ni kwamba… sikutarajia kushinda hii tuzo jioni ya leo, tayari nilikuwa mwingi wa furaha kwa kuwa na wachezaji wenzangu jioni ya leo na kushinda tuzo hii ni jambo jingine la kufurahisha zaidi.
“Hii ni siku ya kipekee kwangu na nataka kuifurahia na wachezaji wenzangu na kuwashukuru kwa sababu bila ya wao nisingeweza kuwa hapa, pia ningependa kufurahia tuzo hii na watu niwapendao, ambao wamekuwa wakiniunga mkono na wakati wote wamekuwa pamoja name.
“Pia napenda kufurahia tuzo hii na kutoa shukrani kwa timu nzima ya Barcelona na Argentina,’’ alisema Messi.
Hii ilikuwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa tuzo ya Ballon d’Or, mwaka 1956 kuunganishwa na tuzo ya Fifa ya mwanasoka bora wa mwaka wa dunia, ambayo Fifa iliianzisha mwaka 1991, hiyo maana yake ni kwamba safari hii Messi alichaguliwa na waandishi wa michezo duniani kote, pamoja na makocha na manahodha wa mataifa 208.
Messi alinyakua pointi 853 ambayo ilikuwa ni asilimia 22.65 ya kura zote akifuatiwa na Andres Iniesta asilimia 17.36 na Xavi Hernandez asilimia 16.48.
Akiwa ndio kwanza ana miaka 23, Messi alikuwa mchezaji mdogo kushinda taji la pili la Ballon d’Or ingawa uteuzi wa mshindi uliibua malalamiko.
“Ningependa kuangalia vigezo vinavyohitajika kumpata mshindi wa Ballon d’Or…Kombe la Dunia limekuwa kitu muhimu katika tuzo za aina hii isipokuwa kwa mwaka ambao Hispania imeshinda,” alisema kipa na nahodha wa Real Madrid na timu ya Taifa ya Hispania, Iker Casillas.
“Kitu pekee sasa ninachoweza kusema ni hatuna bahati, Wahispania wote wanaona kama hawakubaliani, ningependa kuona Andres au Xavi anashinda lakini tutaendelea kupambana ili siku moja nao washinde.”
Pia vyombo vya habari karibu vyote vya Hispania (isipokuwa Catalonia) vilililamikia uteuzi wa mshindi kama ilivyokuwa kwa vile vya Italia na Ufaransa, Messi Nooo! Kilisomeka kichwa cha habari cha Gazetta dello Sport, ikiwa ni sehemu ya malalamiko yalyotolewa na vyombo vya habari vya Italia.
Kwa magazeti mengine makubwa ambayo tayari yalimtangaza Andres Iniesta kuwa ndiye mshindi, kitendo cha Iniesta kushika nafasi ya pili walikipokea kwa mshangao, “Haiwezekani na si haki”. Ni kwa sababu haitoi picha ya nani hasa alikuwa mchezaji bora wa mwaka 2010.
Messi na mabao yake 58 ya msimu uliopita yaliyoiwezesha Barca kushinda taji la pili mfulululizo la La Liga na Super Cup baada ya kuifunga Sevilla, haikuonekana lolote ukiongezea na jinsi alivyouanza vizuri msimu mpya (na mabao 28). Kubwa lililoangaliwa na wengi ni Kombe la Dunia pamoja na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Bahati iliyoje, shaka zote ziliondoka mwaka uliofuata, Januari 9, 2012 hakukuwa na malalamiko yoyote Messi alipotangazwa kuwa mshindi wa Ballon d’Or kwa mara nyingine, hiyo ni baada ya kuwa na miezi 12 mizuri katika soka.
Kwa tuzo yake ya tatu mfululizo akawa ameungana kwa tuzo hiyo na kina Michel Platini (1983, 1984, 1985) Johan Cruyff (1971, 1972, 1974) na Marco Van Basten (1988, 1989, 1992) akaingia kwenye kundi la heshima ya kihistoria. Hakuna aliyepiga ‘hat trick’ kama hiyo akiwa na miaka 24.
Katika mchuano wa tuzo hiyo nyuma ya Messi alikuwa Ronaldo na Xavi akaibuka wa tatu.
Itaendelea Jumanne ijayo…