Buswita, Makame kupelekwa kamati ya maadili

Buswita, Makame kupelekwa kamati ya maadili

Muktasari:

  • WACHEZAJI sita wa Polisi Tanzania wanatarajia kupelekwa kwenye Kamati ya Maadali kutokana na makosa ya utovu wa nidhamu.

WACHEZAJI sita wa Polisi Tanzania wanatarajia kupelekwa kwenye Kamati ya Maadali kutokana na makosa ya utovu wa nidhamu.

Wachezaji hao akiwamo Pius Buswita na Abdullazizi Makame na wengine wanne walisimamishwa kwa muda usiojulikana kutokana na kosa hilo ambapo uongozi wa klabu hiyo umeamua kuchukua hatua hiyo kwasasa.

Mbali na hao, wengine ni Rashid Juma anayeichezea timu hiyo kwa mkopo akitokea Simba ambaye anadaiwa kuondoka kambini bila ruhusa ya viongozi wake na kwenda kwenye harusi ya kaka yake ambaye hakurudi kambini hadi adhabu hiyo inatolewa.

Pia kuna George Mpole, Tariq Seif na Abdulmalick Adam ambapo Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo Robert Munisi alisema wachezaji hao watapatiwa barua zao kisha wataitwa katika kamati ya maadili ya klabu kujieleza na baada ya hapo ndipo uamuzi utatolewa.

“Tumewajulisha Simba na Yanga kuhusu wachezaji wao Rashid na Makame, sasa labda wamewachukua wachezaji wao lakini tumewaambia hawako kambini kwetu na hatujui wako sehemu gani

“Siyo kwamba hatuwataki, tunachotaka waende kwenye kamati ya nidhamu wakajieleze, sidhani kama kuna mtu mkubwa kuliko klabu,” alisema Munisi.

Alisema hakuna upungufu ambao utajitokeza baada ya wachezaji hao kusimamishwa kwani wana wachezaji 60, ambapo 30 wamesajiliwa na wengine ni wa timu ya vijana chini ya miaka 20 hivyo hata wakiondoka hakuna tatizo.

Alisema wachezaji kwa ujumla inatakiwa wazingatie nidhamu kwani soka la sasa siyo ridhaa, kwasababu wanalipwa mishahara, posho na haki zao nyingine.