Black Sailors yapanda ZPL kibabe
Muktasari:
- Timu hiyo imerahisishiwa safari yake hiyo kwa kuifunga Ujamaa bao 1-0 katika mchezo uliochezwa Mei Mosi, 2026, kwenye Uwanja wa Mao Zedong, huku mechi ya New City na Taifa Jang’ombe ikimalizika kwa suluhu.
TIMU ya Black Sailors, imefanikiwa kupanda daraja kushiriki Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) baada ya kufikisha pointi 65 katika Ligi Daraja la Kwanza Kanda ya Unguja.
Timu hiyo imerahisishiwa safari yake hiyo kwa kuifunga Ujamaa bao 1-0 katika mchezo uliochezwa Mei Mosi, 2026, kwenye Uwanja wa Mao Zedong, huku mechi ya New City na Taifa Jang’ombe ikimalizika kwa suluhu.
Wakati Black Sailors ikikata tiketi hiyo, Raskazone inayoshika nafasi ya pili imefakisha pointi 59 baada ya kuisulubu Muungano Rangers kwa mabao 3-1.
Raskazone inafukuzia nafasi moja kuungana na Black Sailors ambayo imeshapanda daraja ikihitaji kufikisha pointi 65 ambapo kwasasa ipo nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Daraja la Kwanza Unguja.
Mchezo mwingine uliochezwa uwanja huo majira ya saa 10:00 jioni, ZAFSA iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kundemba.
Ushindi huo unaipa matumaini ya kujiweka katika mazingira mazuri ya kutoshuka daraja ikiwa na pointi 24 ikishika nafasi ya 13, wakati huohuo ikikatisha matumaini ya Kundemba juu ya safari yake ya kupanda daraja msimu huu.
Kwenye Uwanja wa Kinyasini, timu ya Inter Zanzibar iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Sebleni, ushindi ambao unaongeza matumaini ya timu hiyo kuendelea kufanya vizuri katika mashindano hayo.
Katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Tazari, Sharpboys ililazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Urafiki.