Beki Yanga ala shavu Ghana

CHAMA cha soka Ghana (GFA) kimemteua beki wa zamani wa Yanga, Joseph Zutah kuwa meneja mkuu wa vituo vyote vya soka nchini humo kuanzia juzi.

Mafanikio ambayo Zutah ameyapata katika klabu ya Medeama ambayo alikuwa Mtendaji Mkuu kwa kuiongoza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu nchini humo msimu uliomalizika huku pia akiwa makamu wa Rais wa Chama cha wanasoka wa kulipwa Ghana, yameishawishi GFA kumpa fursa hiyo.

Jukumu kubwa la Zutah ni kusimamia ujenzi wa vituo vingi vya soka kwa vijana wadogo lakini pia kuandaa mkakati wa kuviwezesha vituo hivyo kiufundi, pia usimamizi wa mfumo wa uskauti na maendeleo ya kisoka kwa vijana hao.

Zutah mwenye umri wa miaka 29, aliwahi kusajiliwa na Yanga mwaka 2015 na kuitumikia kwa mwaka mmoja kabla ya kuachana nayo na kurejea Ghana kuitumikia Medeama ambayo aliichezea hadi pale alipostaafu Februari mwaka jana.

Beki huyo aliwahi kushinda ubingwa wa Ligi Kuu Ghana na Tanzania Bara kwa nyakati tofauti alizozitumikia Yanga na Medeama akitumika kama beki wa pembeni na wakati mwingine kiungo.

Uongozi kwa Zutah haujamfikia kwa bahati mbaya kwani ni msomi wa elimu ya shahada ya Sayansi na hisabati aliyoipata Chuo Kikuu cha Cape Coast.