Barnabas atangaza vita mpya Transit Camp
Muktasari:
- Msimu huu katika Ligi ya Championship, kikosi hicho cha maafande wa Transit Camp kinashika nafasi ya tano na pointi 46, baada ya kushinda mechi 14, sare nne na kupoteza tano, huku kikifunga mabao 35 na kuruhusu 23.
KOCHA wa Transit Camp, Vicent Barnabas amesema ataendelea kusimamia malengo ya timu hiyo ya kuhakikisha inapanda Ligi Kuu Bara msimu ujao licha ya ushindani mkubwa uliopo Ligi ya Championship, hususan mechi hizi za mwishoni.
Akizungumza na Mwanaspoti, Barnabas amesema licha ya ushindani kutoka kwa wapinzani wao wakubwa, ila bado hawajakata tamaa kwa mechi zilizobakia kwa sababu hakuna timu yenye uhakika wa kushinda nyumbani au ugenini.
"Mechi zilizobakia ni za hesabu zaidi kwa sababu kila timu inahitaji nafasi fulani kutokana na malengo iliyojiwekea tangu mwanzo, wapinzani wetu wa juu wamekuwa na mwenendo mzuri, japo tutaendelea kupambana nao hadi mwisho," amesema Barnabas.
Awali, Barnabas alikuwa ni kocha msaidizi na alipewa majukumu hayo baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Shadrack Nsajigwa 'Fuso' kujiunga na Tanzania Prisons, akichukua nafasi ya Mkenya Zedekiah 'Zico' Otieno.
Barnabas ni miongoni mwa makocha wenye rekodi za kuvutia katika soka la Tanzania na aliipa timu ya vijana ya Mtibwa Sugar chini ya miaka 20, mataji matano mfululizo, kuanzia mwaka 2018 hadi 2022, baada ya kuichezea pia kwa mafanikio.
Kabla ya kujiunga na kikosi hicho cha maafande wa Transit Camp msimu uliopita wa 2024-2025, Barnabas aliipa pia ubingwa timu ya vijana ya Yanga chini ya miaka 17, baada ya kuachana na Mtibwa Sugar, akiendeleza rekodi bora kwa kila timu anayofundisha.
Msimu huu katika Ligi ya Championship, kikosi hicho cha maafande wa Transit Camp kinashika nafasi ya tano na pointi 46, baada ya kushinda mechi 14, sare nne na kupoteza tano, huku kikifunga mabao 35 na kuruhusu 23.