Bao la usiku lailaza hoi Prisons

Mbeya. Bao la dakika za nyongeza lililofungwa na Peter Mapunda limewawezesha Mbeya City kuondoka na alama tatu muhimu dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa dimba la Sokoine jijini hapa.

Mchezo huo ulikuwa wa kwanza kwa timu hizo za jijini Mbeya ambapo licha ya kila upande kupambana kutafuta bao, lakini hadi Prisons haikuamini kilichowakuta.

Hata mashabiki wa Wajelajela hao waliokuwapo dimbani hapo wakiwa na matumaini ya kuamburia alama moja, waliondoka wameshika vichwa baada ya dakika 90 kumalizika.

Hata hivyo licha ya matokeo hayo, lakini Mbeya City watajilaumu sana kutokana na kushindwa kutumia vyema nafasi za wazi walizopata kwa dakika tofauti ambazo zingeweza kuwapa faida na kuondoka na ushindi wa zaidi ya bao hilo.

Katika kipindi cha kwanza Mbeya City walikosa mabao kupitia kwa Eliud Ambokile dakika ya 16 na 50 kisha Juma Luizio naye akakosa dakika ya 24 huku Prisons nao wakijaribu kutengeneza mashambulizi lakini hayakuwa na faida.

Matokeo hayo yanaifanya Mbeya City kuandika rekodi dhidi ya ndugu zao hao kwani msimu uliopita timu hizo hazikufungana kwa mechi zote.