Baleke gumzo kwa beki Dodoma

BEKI wa kati wa Dodoma, Augustino Nsata amesema mshambuliaji wa Simba, Jean Baleke anajua sana soka na aliwapa wakati mgumu wa kumkaba.

Amesema mashabiki wa Simba wasubirie mambo makubwa zaidi kutoka kwa mshambuliaji huyo pindi atakapoizoea ligi ya Bongo.

Juzi katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika katika Uwanja wa Jamhuri Jijini hapa ulimazika kwa Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0, lilowekwa kambani na Baleke dakika ya 45.

Nsata ambaye alipewa jukumu la kumkaba Baleke, alisema mshambuliaji huyo aliwapa wakati mgumu kumkaba kutokana na kuwa msumbufu na kutafuta nafasi za kupewa mpira ili afunge mara kwa mara tofauti na washambuliaji wengine.

“Tunakiri ni mchezaji mzuri na pia alitupa ugumu kwa sababu hatukumfuatilia kwenye ligi, ndio mechi yake ya kwanza hapa Tanzania na sisi tuliwasoma wachezaji wengine tofauti na yeye.

“Ni mtu ambaye tulikuwa hatujajua tumkabe vipi na naamini akija kuzoea ligi yetu ni mchezaji mzuri sana, ana tachi nzuri, anajua kujiweka kwenye nafasi na ni mtu ambaye hakati tamaa, anafuatilia mpira mpaka mwisho.

“Itoshe kusema Simba wamepata mtu yule ni mchezaji mzuri atawaongezea kitu na tutarajie kumwona akifanya vizuri zaidi,” alisema beki huyo ambaye katika mchezo huo alikuwa nahodha. Akiuzungumzia mchezo alisema : “Tulikuwa tunahitaji kushinda ndio maana unaona tulicheza kwa kujituma ila lazima ukubali Simba ni timu kubwa licha ya kwamba tulicheza vizuri lakini wao ndiyo waliopata matokeo."