Aussems, Migne waiteta Simba

Muktasari:

KOCHA wa zamani wa Simba, Patrick Aussems ameweka wazi kwamba kuna kila dalili anahisi Kocha Mfaransa, Sebastian Migne anakuja Yanga.

KOCHA wa zamani wa Simba, Patrick Aussems ameweka wazi kwamba kuna kila dalili anahisi Kocha Mfaransa, Sebastian Migne anakuja Yanga.

Aussems ambaye kwa sasa yuko AFC Leopards ya Kenya, alisema akiwa katika majukumu yake alipokea simu kutoka Ufaransa kwa kocha, Migne ambaye alimuuliza mambo mengi ambayo yanayohusu Tanzania haswa Yanga ambayo Mwanaspoti limejiridhisha kwamba anajiunga nayo wikiendi hii.

Alisema; “Migne niliwahi kuishi naye Ufaransa na baada ya kupata dili hilo la kuja Yanga alinihusishwa kwa kuniuliza kuhusu klabu hiyo pamoja na ligi za Tanzania.”

“Nimefundisha Tanzania na naifahamu Yanga nikamueleza ni timu kubwa ambayo kila msimu ina malengo ya kutwaa ubingwa wa mashindno ya ndani na kucheza mashindano ya kimataifa,” alisema.

“Nilimueleza Yanga kutokana na ukubwa wake pamoja na malengo ya kufanya vizuri kwa kushinda kila mechi iliyokuwa mbele yake ina presha nyingi kutoka sehemu mbalimbali kwa kutokubali kuona wanapata matokeo mabaya.

“Ushindani mkubwa Yanga wanaupata kutoka kwa Simba ambao ni timu niliyokuwa naifundisha kwa wakati nipo Tanzania nilimueleza pia hilo,” alisema.

Katika hatua nyingine, Aussems alisema alimueleza Migne ligi ya Tanzania inakuwa na ushindani kwani kila timu huwa inatamani kupata matokeo mazuri dhidi ya timu kubwa kama Yanga.

Aussems kikosi cha Yanga kinawachezaji wazuri kutokana na malengo yake wanaweza kufanya mambo mbalimbali ambayo kocha atakuwa anayahitaji ili kufikia kile ambacho wamekipanga mwisho wa msimu.

“Sikuficha kumpa baadhi ya changamoto hata ambazo nimekutana nazo hapa Tanzania lakini hata yeye pia anatakiwa kujindaa anaweza kukutana nazo au ikawa tofauti na hivyo,” alisema Aussems.

Yanga bado hawajatangaza kocha mpya ambaye atakuja kuchukua mikoba ya Mrundi Cedrick Kaze lakini Mwanaspoti linafahamu Migne ndiye Kocha Mkuu mpya na wameshamalizana kila kitu na hata ameshapiga simu kambini kuzungumza na Juma Mwambusi na baadhi ya wachezaji wa kigeni.