Simba, Azam kimenuka
UNGUJA. KOCHA wa Azam, Abdihamid Mohammed amesema yupo tayari kuwavaa Simba na itakuwa ni fainali nzuri na ya kuvutia ambayo wanakwenda kubeba ndoo.
“Unapokuwa kwenye mashindano yoyote unapaswa kuwa na utayari wa kucheza na timu yoyote ama kupokea aina yoyote ya matokeo kama ilivyo sasa kuwa tunawasubiri Simba na tutashinda kwani hakuna anayeingia uwanjani akihitaji kufungwa.
“Tunaenda kukutana na timu bora na yenye ushindani, lazima tuipe heshima Simba lakini hata sisi ni bora na tutafanya vizuri kwani makosa tuliyoyaona tutayafanyia kazi, tupo tayari,” alisema Mohammed Kocha huyo aliyerejesha morali kikosini.
Lakini kocha wa Simba Pablo Franco alisema kuwa; “Kadri siku zinavyokwenda kwenye mashindano haya wachezaji wangu wanaimarika zaidi hivyo hata fainali tutafanya mambo makubwa zaidi ya haya.”
“Wachezaji wangu wamecheza vizuri sana ukilinganisha na mechi zilizopita hatua ya makundi, wapinzani wetu sio kwamba walikuwa wabaya ila tulikuwa bora zaidi yao, tunaenda kucheza na Azam ambayo pia ni timu imara lakini naamini tutashinda maana ndiyo lengo letu ingawa yanatusaidia kuwa fiti zaidi kuelekea michuano yetu ya kimataifa,” alisena Pablo. Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ kocha wa Namungo alisema kuwa; “Unapocheza na timu bora tarajia kufungwa, Simba ni timu bora na wamecheza vizuri kuliko sisi, wachezaji wangu wamefungwa mabao yote ya kizembe, Simba walimikili mpira kwa kiasi kikubwa hivyo hii ni fainali lazima mshindi apatikane. Kuna mapungufu madogo madogo tu ambayo tunaenda kuyafanyia kazi maana hatujafanya mazoezi na tangu tujiunge nayo.”